Habari rafiki yangu kwa siku hii nyingime mzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

IMG_20170102_073855
Tutumie nafasi hii ya leo vizuri ili tuweze kufanya makubwa.
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambao tunaweza kufanya makubwa zaidi kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kuhakikisha wewe mwenyewe.
Watu wengi huangushwa na wale watu ambao wanawaamini sana.
Wengi huingizwa kwenye hasara na wale watu ambao wanaamini wanaweza kufanya vizuri bila uwepo wao.
Na hata kwenye kutapeliwa na kudhulumiwa, kunaanza na kuamini.
Hivyo basi, kama tunataka kuepuka yote haya, tunahitaji siyo tu kuamini, bali kujihakikishia sisi wenyewe juu ya kile tunachoamini, kudhibitisha sisi wenyewe.
Kama ni mtu anafanya kitu, usiishie tu kuamini atafanya vizuri, bali fuatilia kwa karibu na hakikisha amefanya vizuri kweli. Dhibitisha amefanya kweli na siyo kuishia kuamini tu.
Hata pale mtu anapokupa wazo jipya, au fursa mpya, usikubali tu kwa sababu unamwamini mtu huyo, badala yake jihakikishie wewe mwenyewe, dhibitisha kama ni kweli kile ambacho mtu anakuambia.

Wengine watakuambia huniamini hata mimi?
Na mwambie ni utaratibu wako kujihakikishia kabla ya kuchukua hatua, ili kuzuia kufanya makosa yatakayokugharimu.
Wakati mwingine watu wanaweza kukuingiza kwenye matatizo bila hata ya wao wenyewe kujua. Hivyo utaratibu wa kujihakikishia mwenyewe, utakuokoa na hilo.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.