Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

IMG_20170102_073855
Tuitumie siku ya leo vizuri iki tuweze kusogea karibu na ndoto za maisha yetu.
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA tunaweza kufanya makubwa kwenye maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu muda ni sasa.
Kama kuna hatua yoyote unataka kuchukua kwenye maisha yako, huna wakati mwingine zaidi ya sasa.
Tumekuwa tunajidanganya sana na kesho, lakini kesho imekuwa haifiki.
Muda tulionao ni huu tulionao sasa, huu ndiyo muda ambao tuna uhakika nao.
Huu ndiyo muda ambao tunaweza kuutumia kufanya makubwa.
Lakini akili zetu hazipendi miili yetu itumie nguvu zetu kwa sasa, hivyo hutudanganya kwamba tunaweza kufanya kesho,
Kesho ikifika inakuwa tena kesho…
Inaenda hivyo miaka na miaka, mpaka siku moja unastuka muda umekwenda na hujachukua hatua.
Sasa unahitaji kubadili hilo, kwa makusudi kabisa.
Kama kipo kitu muhimu kufanya, kipange kabisa utakifanya siku gani na muda gani,
Itakapofika muda huo, usisikilize kile kinachokuambia utafanya kesho, hakikisha kuna hatua unaichukua ili kuweza kufika kule unakotaka.

Ukiendekeza hizi kesho rafiki, utakuja kujichukua mwenyewe, kwa kujiona ulikuwa mzembe, kumbe hukua mkali juu yako mwenyewe.
Anza kuwa mkali kwako, usikubali kirahisi pale akili yako inapokuambia kesho ipo, anza mgomo na chukua hatua sasa.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.