Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ni msingi muhimu sana kwetu kwa mafanikio.
Asubuhi ya leo tutafakari sababu ya watu kukukatisha tamaa.
Iko hivi rafiki, huwezi kuanza kufanya jambo lolote kubwa kwenye maisha yako, wasijitokeze watu wanaojitolea kukushauri, bila hata ya wewe kuwaomba ushauri.
Na katika hao, wapo watakaokuambia achana na hicho unachopanga kufanya.
Watakuambia acha kujisumbua, hutaweza, wengine wameshindwa.
Na zaidi watakuambia kwa nini unajihangaisha sana?
Watu hawa wanakuambia hivyo siyo kwa sababu yako, ila kwa sababu zao binafsi.
Kwa sababu hawakujui wewe, wala hawajui uwezo mkubwa uliopo ndani yao.
Lakini wanajijua wao, kwa uwezo wao, au uvivu wao, wanaona hawawezi kufanya kile wanachofanya.
Lakini mwingine akikifanya, itawaaibisha wao, itawafanya wao waonekane wazembe, na wao hawataki hilo, hivyo watakazana kwa namna yoyote ile, ili kuhakikisha hakuna anayefanya.
Kwa sababu kama wote hawajafanya, basi hakuna mzembe.
Lakini wewe ukiweza, moja kwa moja wao ni wazembe.
Hivyo rafiki yangu, yeyote atakayejitolea kukupa ushauri wa kukatisha tamaa, kwanza angalia yeye amefanya nini kikubwa kama unachotaka kufanya wewe.
Halafu pili mpige maswali mpaka akimbie mwenyewe, kama utakuwa na muda huo. Mwulize yeye binafsi anajuaje kuhusiana na hicho unachofanya wewe. Amewahia kukifanya? Waliofanya wakashindwa anajua ni kwa nini? Mpe mifano ya walioweza kufanya, mwulize wale wana nini?
Mwisho kabisa, mwambie atumie nguvu hiyo ya kukatisha watu tamaa kufanya jambo ambalo linaonekana, na siyo kutoa maneno maneno tu.
Sijawahi kuona mtu aliyefanya makubwa, akimkatisha tamaa mwingine asifanye. Ila wale ambao hawajawahi kufanya lolote kubwa, ndiyo vimbelembele wa kukatisha wengine tamaa.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.