Linapokuja swala la falsafa, wengi hujiweka pembeni kwa kuamini kwamba hicho ni kitu cha watu fulani. Watu fulani ambao wamekaa darasani na kufundishwa miaka mingi mpaka kuwa wanafalsafa.

Au kama ilivyo cheo cha elimu cha PhD ambacho ni shahada ya uzamivu, au udaktari wa falsafa. Kwa mtazamo huu wengi wamekuwa wanajiweka mbali na falsafa, na kuona haiwahusu. Wao kinachowahusu ni yale maisha yao ya kila siku, hawana muda na falsafa. Na hapa ndipo watu wanapofanya makosa makubwa sana ya maisha yao.

Falsafa siyo cheo au aina ya elimu ambayo mtu anaipata, bali falsafa ni aina ya maisha ambayo mtu anachagua kuishi. Falsafa ni jinsi ambavyo unachagua kuishi maisha yako, jinsi unavyopambana na changamoto zako, na jinsi unavyohusiana na wengine.

Huhitaji cheti ili uwe mwanafalsafa, wala huhitaji watu wakudhibitishe wewe kama mwanafalsafa, bali unahitaji kuchagua namna ya kuyaishi maisha yako ambayo itayafanya maisha yako kuwa bora sana.

Kabla ya kuwepo kwa mfumo rasmi wa elimu, elimu kuu iliyokuwa ikitolewa miaka zaidi ya 3000 iliyopita, ilikuwa elimu ya falsafa. Ukifuatilia falsafa nyingi, utaona enzi za utawala wa Roma, walikuwepo watu ambao walichagua aina ya falsafa wanayoweza kuishi nayo. Na wengine walipenda falsafa hiyo na kujiunga nayo.

Ni katika kipindi hicho ambapo nguvu ya falsafa ilianza kuonekana na kuonekana kuwa tishio kwa watawala. Hivyo wanafalsafa wengi waliuawa, mfano Socrates, Cato, Seneca na wengine wengi. Waliuawa na wengine walilazimishwa kujiua kwa tuhuma za kuwaharibu vijana.

Falsafa ilionekana kuwaharibu vijana kwa sababu iliwafanya wafikiri kwa kina na kuweza kuhoji, kitu ambacho ni sumu kwa utawala wowote ule. Utawala wowote haupendi watu wafikiri sawa sawa au kuhoji, wanapenda watu wawe wanashangilia tu na kukubali kila kitu ili kazi yao iwe rahisi. Hivyo akiwepo mtu anayewafundisha watu namna ya kufikiri na kuhoji, anakuwa hatari kwa utawala.

Hizo ni enzi za zamani, ambazo zinaweza zisifanane sana na sasa, lakini ukweli unabaki kwamba falsafa ina nguvu kubwa. Falsafa ina nguvu ya kuweza kumpatia mtu uhuru wa maisha yake kwa kumwezesha mtu kufikiri sawasawa. Na pia inamwezesha mtu kuishi maisha yanayoendana na kile anachoamini, maisha yenye maana kwake na siyo ya kuiga au ya kufuata mkumbo

Hii ni nguvu kubwa ya falsafa ambayo inapatikana kwa kila mtu.

Kila mtu anaweza kuwa mwanafalsafa, kama atachagua kuwa. Kila mtu anaweza kutumia akili yake kufikiri vizuri zaidi na akaweza kutoka pale alipo.

Silaha kubwa ambayo sisi binadamu tunayo, ambayo viumbe wengine hawana, ni namna ya kufikiri. Simba ni mkali sana na hatari, lakini tunaweza kumkwepa na hata kumwinda kwa sababu tunaweza kufikiri na kuja na njia mbalimbali. Wakati yeye simba hawezi kufikiri tofauti na mazingira yake, ana namna fulani ya kuishi ambayo ataishi hivyo hivyo miaka yote.

Pamoja na silaha hii kubwa tuliyonayo, wapo watu ambao wamechagua kuficha silaha hiyo na kwenda kama kondoo, hawataki kufikiri, wametoa kazi hiyo ya kufikiri kwa wengine, wafanye kile wanachotaka. Na wao wanaishia kulalamika na kulaumu.

Hapa ndipo utawasikia watu wakilalamika kwamba serikali haijawasaidia au haiwajali, kama vile kuna mkataba ambao walisaini na serikali kwamba ni jukumu la serikali kuhakikisha maisha yao ni mazuri.

Wengine utawakuta wapo kwenye ajira miaka zaidi ya 10, hawapendi kazi hiyo, haiwalipi vizuri, lakini kila siku wapo na kila siku ni malalamiko. Kila siku ni kusema wale ambao wamefanikiwa kwenye kazi hiyo, labda ambao wapo juu yake kwa kuwa wananufaika zaidi. Utafikiri mtu huyu alipozaliwa alikabidhiwa kazi hiyo kwamba lazima afe nayo.

Bado wale ambao utawakuta kila siku wanahamahama kwenye kile wanachoamini, labda ni dini au hata siasa. Leo yupo hapa, akikosa kile alichofikiri angepata, anaondoka na kwenda kwingine, ambapo anafikiri atapata kile anachotaka. Anazunguka na kumaliza kote, lakini hapati anachotaka.

Wengine wengi utawakuta wanaishi maisha ambayo kila kitu wanalalamikia, lakini hawachukui hatua.

Kukosa falsafa imara kwenye maisha, kumewafanya wengi sana kuwa na maisha ambayo hawayaelewi, au maisha ya kusadikika. Mfano pale mtu anapoambiwa na wanasiana nipe kura na nitafanya maisha yako kuwa bora, anatoa kura halafu anasubiri maisha yawe bora. Anakubali kuishi maisha ya kusadikika, anaweza uwezo wake wa kufikiri mfukoni na kufuata wengine wanafanya na kusema nini.

Ndiyo maana ninakutaka sana wewe rafiki yangu, ujifunze falsafa, jifunze falsafa kupitia makala hizi za FALSAFA MPYA YA MAISHA ili uweze kufungua uwezo wako wa kufikiri, ili uweze kuona mambo kama yalivyo na siyo kama watu walivyotegesha uone. Uweze kufanya maamuzi sahihi ya maisha yako na kuyasimamia.

Na muhimu zaidi kwenye falsafa, uweze kuchagua aina ya maisha unayoishi, na uende nayo. Muhimu kabisa, usikazane kuwaambia watu kwamba wewe ni mwanafalsafa, haitakusaidia wewe wala wao, lakini kadiri unavyoendesha maisha yako, watu watakuona wewe ni wa tofauti na watapenda kujifunza zaidi kupitia wewe, hapo ndipo unapoweza kuwakaribisha kwenye maisha ya falsafa.

Tumeshajifunza mengi kwa namna ya kuyapeleka maisha yetu kwa njia ya falsafa. Mambo muhimu ya kuzingatia, namna ya kupambana na changamoto ngumu na kadhalika. Kala kuna makala za falsafa ambazo hukupata nafasi ya kuzisoma, basi zote zipo hapa, bonyeza maandishi haya kuzisoma.

Nakusihi sana tuendelee kujifunza pamoja falsafa, na siyo tu kujifunza bali iishi falsafa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.