Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora zaidi.

IMG_20170102_073855
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, msingi unaotuwezesha kufanya makubwa.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUKAZANA KUPOTEZA MAISHA….
Kama hujui ni wapi unapokwenda, njia yoyote itakuwa sahihi kwako, na pia utafika popote.
Kukazana kuweka mbio, wakati hujui ni wapi unakwenda, ni kukazana kupotea, na mbaya zaidi kukazana kupoteza maisha.

Kitu chochote unachofanya, kama hujui unachotaka hasa ni nini kwenye kitu hicho, basi unakazana kupoteza maisha. Kwa sababu unaweka muda pale, muda ambao hautakuja kuupata tena.
Na muda rafiki, ndiyo maisha yenyewe.

Kufanya kitu ambacho hujui unataka nini hasa, au hujui kwa nini unafanya, ni kuchagua wewe mwenyewe kuharibu muda wako na kupoteza maisha yako. Huku ukiwa umeyaacha yale muhimu kwako kufanya.

Kuepuka kupoteza maisha, na kuhakikisha unafika kule unataka kufika, jua nini unataka kwenye kila unachofanya.
Usifanye tu kwa sababu kila mtu anafanya,
Usifanye tu kwa sababu jana ulifanya,
Na wala usifanye kwa sababu unataka kuonekana unafanya.
Fanya kwa sababu unajua wapi unataka kufika na unachofanya kitakufikisha pale.
Siyo lazima ufanye kile ambacho kila mtu anafanya.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Nenda KATHUBUTU, UKASHINDE NA USHUKURU.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.