Wastoa wa roma ndiyo waliochangia sana ukuaji wa falsafa ya ustoa. Japo wapo wanafalsafa wengi wa roma, wanne wamekuwa na mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa falsafs hii.

Wa kwanza alikuwa Seneca, huyu ni mstoa aliyetambulika kwa kuandika sana. Ndiye mstoa ambaye maandiko yake mengi yamepona mpaka sasa. Aliandika vitabu vingi na pia aliandika barua nyingi za kifalsafa kwa rafiki yake Lucilius ambaye alikuwa akimshauri namna ya kuishi maisha yenye furaha.
Licha ya falsafa, Seneca pia alikuwa mwandishi wa maigizo, na pia mwekezaji, ambaye alikuwa tajiri sana.
Alikuwa pia mshauri wa karibu wa mtawala wa roma aliyeitwa Nero, ndiye aliyemfundisha tangu akiwa mdogo.
Seneca aliwekwa vizuizini na baadaye kulazishwa kujiua kwa tuhuma za kutaka kupindua uongozi wa Roma.

Wa pili alikuwa Rufus ambaye yeye hakuandika sana, bali alikiwa akiwafundisha watu namna ya kuishi, namba ya kula na namna ya kupeleka maisha yao kama wastoa.

Wa tatu alikuwa Epictetus, huyu alikuwa mtumwa, ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye makazi ya mtawala wa roma. Hapo alionesha uelewa wake mkubwa na hivyo kupata fursa ya kujifunza zaidi. Baada ya mtawala kufa, alipata uhuru na kwensa kuanzisha shule yake ya falsafa na kufundisha ustoa. Yeye aliweka mkazo zaidi namna ya kuwa na maisha yenye utulivu. Aliandika kitabu ambacho wengi walikuwa wakikitumia kama mwongozo wa maisha.

Wa nne ni Marcus Aurelius, huyu alikuwa mtawala wa Roma, alianza kujifunza falsafa tangu akiwa mdogo, na alipoingia madarakani aliendelea kuishi kwa falsafa. Aliweka mkazo zaidi kwenye maadili.
Na licha ya kuwa mfalme, na mwenye nguvu, hakulazimisha mtu yeyote kujifunza ustoa, wala hakuwahi kumwambia yeyote kwamba yeye ni mstoa. Aliishi maisha ya ustoa na alikuwa na jarida lake la kila siku ambapo aliandika kila alilojifunza kwenye maisha. Baadaye jariba hili lilichapwa kama kitabu na kuitwa MEDITATIONS OF MARCUS AURELIUS, kitabu ambacho ni maarufu sana kwa ustoa.
Marcus anachukuliwa kama mmoja wa watawala watano bora sana katika utawala wa Roma, licha ya kipindi chake cha uongozi kukubwa na changamoto kama ukame, tetemeko na vita, bado aliweza kusimama na kushinda yote, kwa sababu ya falsafa ya ustoa.

Tunaona namba ustoa unavyomfaa kila mtu na namna tunavyoweza kuutumia kuwa na maisha bora, kuanzia furaha mpaka utajiri.