Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri kuboresha maisha yako. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani leo ni siku bora sana na ya kipekee kwetu hivyo tunaalikwa kutumia siku yetu ya leo vizuri vilivyo, iendee siku yako kwa falsafa ya nidhamu, kujituma na uadilifu.

 

Rafiki, napenda kukushauri kitu kama wewe ni mmoja wa watu wanaoteseka kisaikolojia na kufuatilia kila habari ya matukio yanayoendelea kutokea hapa Tanzania acha mara moja na fuatilia maisha yako, kumbuka hutakuja kupata tuzo ya kufuatilia habari, fuatilia ya kwako kuna kelele nyingi sana huwezi kuzifuatilia zote hivyo changua kitu kimoja tu cha kufuatilia kwenye maisha yako. Usiwe mtumwa wa habari kwani utasahau kufanya ya kwako jaribu kujitenga kidogo na matukio yanayoendelea kutokea hapa kwetu.

Mpendwa rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mambo mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Hivyo basi, nakusihi sana tuweze kusafiri pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo. Katika makala yetu ya leo tutakwenda kujifunza wote kwa pamoja mada inayokwenda kwa kichwa cha habari kinachosema Kitu Ambacho Huwezi Kukikosa Kama Ukikitafuta Kwa Mtu Yeyote Yule.

SOMA; Kama Unatafuta Kazi, Acha Kufanya Makosa Haya Ili Kuipata Kazi Hiyo.

Mpendwa msomaji, aliyekuwa raisi wa awamu ya kumi na sita wa Marekani (16),mwandishi,mwanasiasa na mwanasheria Abraham Lincoln enzi za uhai wake aliwahi kunukuliwa akisema, ‘’those who look for the bad in people will surely find it’’ akiwa na maana ya kwamba, wale wote wanaotafuta ubaya ndani ya mtu hakika wataupata ubaya. Ndugu msomaji, kama wewe unatafuta ubaya au mabaya kwa mtu basi tarajia tu kuupata ubaya huo kwani ukitafuta baya kwa mtu yeyote huwezi kukosa kasoro au ubaya huo.

Ndugu msomaji, mara nyingi sisi binadamu tumekuwa ni watu wa kuangalia mabaya kwa wenzetu, tumekuwa ni watu wa kutafuta mabaya kwa wenzetu kuliko mazuri ndiyo maana mambo kila unayemuona mbele yako unahisi ni mbaya kwa sababu ya kutafuta ubaya. Ukitafuta ubaya kwa jirani yako hakika huwezi kukosa, vivyo hivyo, hata katika mahusiano yetu ukitafuta ubaya kwa mwenza mwako huwezi kuukosa, ukitafuta ubaya kwa marafiki zako huwezi kuukosa hata siku moja. Leo ukiamua kutafuta ubaya kwa Deo Kessy tarajia kuupata kwani huwezi kuukosa.

Mpenzi msomaji, kwa hiyo, kama Abraham Lincoln anavyotualika kama tukitafuta ubaya ndani ya mtu hauwezi kuukosa, tunachukiana kwa sababu ya kutafuta ubaya kwa mtu, unakuta mtu hajakufanyia ubaya unaanza kuutafuta ubaya juu yake kwa njia hii huwezi kuukosa ubaya kwa mtu. Kwa hiyo, badala ya kutafuta ubaya kwa mtu sasa tuanze kutafuta uzuri kwa mtu, tumeona wazi kuwa kama tukitafuta ubaya wa kila mtu hapa duniani hatuwezi kukosa hivyo basi, badala yake tutafute uzuri ndani ya mtu.

SOMA; Vitu Muhimu Usivyotakiwa Kufanya Wakati Mambo Yako Yanapokwenda Vibaya.

Hivyo basi, mwache mtu akabaki na ubaya wake wala usimchunguze, waswahili wanasema ukimchunguza sana bata hutomla, kwa hiyo acha kuchunguza na kutafuta mabaya kwa watu, bali tafuta mazuri tu kwa mtu na ondoka zako. Kama unafaidika na mtu Fulani shukuru na endelea kufaidika naye kwa thamani anayoitoa katika maisha yako. Ukianza kutafuta ubaya kwa watu kila mtu utamwona ni adui, mbaya katika maisha yako, hivyo wewe lenga kutafuta uzuri tu wa kitu Fulani lakini mambo ya kuchunguzana na kutafuta ubaya wewe yaache kwani ukitafuta tarajia kuyapata.

Changamoto kubwa ya kuanza kutafuta ubaya ndani ya mtu huanza kuzaa chuki, wivu na kama tunavyojua chuki huzaa mauti, maisha ya kulipizana visasi nayo yataanza na mambo mengi hasi yataibuka. Kila mtu ana thamani yake ya pekee hapa duniani hivyo ni vema kama ukitafuta thamani aliyonayo mtu kuliko kutafuta ubaya. Maisha ya kutafuta ubaya yanakuja kuzaa upendo wa kipimo na upendo wa kipimo hauna nafasi katika maisha yetu na mtakatifu Augustino, enzi za uhai wake aliwahi kusema kipimo cha upendo ni kupenda bila kipimo.

Hatua ya kuchukua leo, acha mara moja kutafuta ubaya kwa mtu na anza mara moja kutafuta thamani au uzuri wa mtu na unufaike nao. Ukitafuta ubaya kwa mtu yeyote yule huwezi kuukosa na hivyo utatarajia kuupata tu.

Kwa hiyo, tunaaliwa kuishi kwa upendo katika maisha yetu, badala ya kutafuta mabaya kwa watu tunaalikwa kutafuta mazuri kwani unapotafuta mabaya kwa mtu tarajia kuyapata mabaya hayo.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kujifunza zaidi.