Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu WATU WASIOSHAURIKA…
Unaweza kuona mtu anakosea kabisa, kulingana na uzoefu wako, lakini unapomshauri akawa mkali kweli.
Akakuambia nani amekuomba ushauri, au umejuaje na mengine mengi.
Hata kama umetoa ushauri wa kujenga, siyo wote wanaoweza kuupokea ushauri huo.
Hivyo kabla hujakimbilia kushauri watu, lazima ujue kwanza kama mtu huyo anashaurika ama la.
Kwa upande wako pia, usiwe mtu usiyeshaurika, kwa sababu utakosa mazuri kwenye maisha yako.
Sikiliza wanaokushauri, usijibu vibaya wala usiwakatishe tamaa.
Uzuri wa ushauri ni kwamba hakuna anayekulazimisha kuufanyia kazi. Unasikiliza lakini maamuzi yanabaki kwako mwenyewe.
Waepuke wasioshaurika na wewe usiwe mtu asiyeshaurika.
Huwezi kujua kila kitu, na usichokijua na kukiona ndiyo kinachokuzuia kufanikiwa.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.