Hasira ni moja ya hisia hasi tunazokutana nazo kutokana na mambo mbalimbali yanayoendelea kwenye siku zetu.
Kwa kuwa wastoa tunapenda kuwa na utulivu, hasira zinavuruga utulivu wetu.
Hovyo wastoa wanatushauri kutoendekeza hasira.
Seneca anasema kwamba hasira ni ukichaa wa muda mfupi, yaani unapokuwa na hasira, huna tofauti na kichaa au mtu aliyerukwa akili.
Ni kwa hasira watu wanagombana, wanauana na hata mataifa yanateketea. Tukiweza kudhibiti hasira zetu, tutajiepusha na mabaya mengi.
Hivyo tunashauriwa kutokuwa na hasira, na kama hasira ikitujia basi tuwe na njia za kuondokana na hasira mara moja kabla hazijaleta madhara kwetu.
Na wastoa wanatupa mbinu mbalimbali za kuondokana na hasira.
1. Tuache kuhitimisha na kuamini kwamba kile tulichokosa, au matatizo tuliyopata yamesababishwa na wengine. Badala yake tuone mchango mzuri wa wengine katika kile tunachofanya.
2. Tuache kutaka vitu viwe rahisi, au viwe kama vile tunavyotaka sisi. Mambo tusiyotarajia huwa yanatokea kila mara, kukasirishwa na vitu kaka hivi ni kutokana na kutaka kila kitu kiende kama unavyotaka wewe, jambo ambalo haliwezekani.
3. Vitu vinavyotukasirisha, havituumizi kama kukaa na hasira muda mrefu. Hivyo kukaa na hasira ni kuchagua kujiumiza.
Marcus yeye anatukumbusha kwamba, hayo yanayotukasirisha leo, miaka mingi ijayo hayatakuwa hata na maana.
Anatupa mfano kwamba miaka 100 iliyopita, watu walikuwa wanaoana, wanazaa watoto, wanaishi, wanaoneana wivu, wanagombana na sasa hivi hakuna hata kimoja kati ya hivyo tunakumbuka.
Wastoa wanatushauri pale hasira zinapotujia, basi tusikubali zitupelekeshe. Badala yake tujidhibiti, tutulize akili zetu, tusiseme wala kufanya lolote. Tuyahamishe mawazo yetu na kuyapeleka mbali na kile kinachotukasirisha, na tutaweza kuondokana na hasira.
Maisha yetu ni mafupi sana kuyapoteza kwa kuwa na hasira na mambo ambayo siyo ya msingi.
Wewe kama mstoa, usijiruhusu kuingia kwenye hasira, inakupotezea muda, kukuondolea utulivu na furaha na kukuingiza kwenye matatizo.