Pale tunapopata misiba, hasa ya watu wa karibu kwetu, kama watoto, wazazi na hata ndugu, tunapitia kipindi cha huzuni.
Lakini vipi kwa falsafa ya ustoa? Kwa sababu huzuni ni hisia hasi na wastoa hawakubali kutawaliwa na hisia hasi.
Seneca anatuambia ya kwamba, ni wajibu wetu kuhuzunika, maana hatuwezi kuzuia huzuni. Ila anatuonya tujue wakati gani wa kuacha. Tusiruhusu kutawaliwa na huzuni muda wote. Tunaweza kuhuzunika pale tunapojua mtu wa karibu amefariki au hatutamwona, lakini tusipoteze muda mwingi kwenye hilo.
Seneca anatupa mbinu mbalimbali za kuweza kuimaliza huzuni yetu haraka.
Mbinu ya kwanza ni kutengeneza taswira kwenye fikra zetu, ya namna ambavyo yule aliyefariki alivyokuwa na manufaa kwetu. Badala tu ya kuangalia kwamba ameondoka, tuangalie uwepo wake hapa duniani umetusaidiaje sisi, na hata sisi tuliwasaidiaje wao. Kwa njia hii utapata kitu cha kushukuru na kuacha kuhuzunika.
Mbinu ya pili ni kufikiria yule aliyefariki angechukuliaje hali yetu. Kama kuhuzunika kwetu kunafanya maisha yetu kuwa ya hovyo, tujiulize yule tunayemhuzunikia angetaka maisha yetu yaweje baada ya yeye kuondoka. Kama angependa tuwe na maisha mazuri, basi hatuna haja ya kuhuzunika, badala yake tunahitaji kuwa na maisha mazuri. Na kama alitaka tuwe na maishabya hovyo basi hatuna haja ya kuhuzunika, maana hakututakia mema.
Epictetus yeye anatuasa katika kuwasaidia wale ambao wapo kwenye huzuni, tujichunge sana wasituambukize huzuni zao. Kwa sababu kwa sisi kutumbukia kwenye huzuni, hatuwezi kuwasaidia wengine kutoka kwenye huzuni zao.
Hivi ndivyo tunavyoweza kuishinda huzuni kwa kufikiri kwa kina.