Kama ambavyo tumeona, ni muhimu sana mtu kuwa na falsafa ya maisha, kwa sababu bila ya falsafa, hakuna hatua kubwa mtu anaweza kupiga.
Na kama ambavyo tumejifunza kwenye falsafa ya ustoa, dhumuni kuu la falsafa ya ustoa ni kuwa na utulivu kwenye maisha, kwa kuishi kulingana na asili.
Zipo falsafa nyingi za maisha ambapo watu wanaweza kuchagua. Hakuna falsafa moja ambayo inamfaa kila mtu.
Hivyo hata falsafa ya ustoa, haiwezi kuwa ya kila mtu.
Hivyo kwa maelezo haya kuhusu falsafa ya ustoa, yanapaswa kwanza kumshawishi mtu kuhusu umuhimu wa kuwa na falsafa ya maisha na pili kuhusu falsafa ya ustoa.
Wapo watu ambao tabia na haiba yao inaendana na falsafa ya ustoa, yaani kabla hata hawajaambiwa chochote kuhusu ustoa, tayari wanaishi misingi ya falsafa hii.
Na wapo watu ambao falsafa ya ustoa inapingana na tabia na haiba zao.
Hivyo, katika kufikiria kuifanya falsafa ya ustoa kuwa falsafa ya maisha yako, angalia kama inaendana na tabia na haiba yako. Pia angalia kama inakuwezesha kupata kile ambacho unahitaji sana kwenye maisha, ambacho ni utulivu.
Kama hitaji lako la maisha ni tofauti na utulivu, basi falsafa ya ustoa haitakufaa, hivyo tafuta falsafa nyingine.
Lakini kama unataka utulivu, ba upo tayari kuishi kulingana na sheria za asili, ustoa ni falsafa yako ya maisha.