Dhumuni kuu la wastoa ni kuwa na maisha yenye utulivu.
Lakini utulivu huu unaweza kuvurugwa na wengine.
Hasa pale tunapohitaji kufanya kazi pamoja na wengine ambao tabia zao siyo sawa na zetu.

Hivyo wastoa wanashauri mtu uchague tabia muhimu kwako na kuendesha maisha yako kwa tabia hizo. Na kwa yeyote unayekutana naye kwenye maisha, unakwenda kwa tabia hizo.

Wastoa wanasisitiza haya yafuatayo;
1. Kutojenga urafiki na watu wasio na tabia nzuri, maana hao watatuambikiza tabia zao mbaya.
2. Kujenga urafiki na wale wenye tabia ambazo sisi tunazijenga kwetu pia, hao watatuambukiza tabia hizo nzuri.
3. Kuepuka kukaa na watu ambao muda wao wote ni kulalamika ba kulaumu, hawa wanakuondolea utulivu wako.
4. Kutokufikiria juu ya wengine wanatufikiriaje sisi, badala yake kufanya yale ambayo ni muhimu sisi kufanya.
5. Kutohudhuria sherehe ambazo hazina mantiki, ambazo siyo wajibu wetu kuhudhuria na wanaoziandaa siyo wenye tabia tunazopenda.
6. Kuepuka kuwa mtumwa wa hisia za ngono, tusiendeshwe na hisia hizo za kufanya ngono, badala yake tujidhibiti.

Marcus anatuambia, pale tunapohitajika kufanya kazi au kukaa na watu wanaotukera, njia ya kuondoka na hilo ni kufikiria kwamba hata sisi wenyewe kuna namna tunawakera wengine.
Kama hiyo isipotusaidia, basi tujikumbushe hatutaishi milele, siku siyo nyingi tutakufa na kukerwa kwetu na wale wanaotuzunguka kutakuwa kumefika mwisho.