Lengo kuu la ustoa ni kuwa na maisha yenye utulivu, kuwa na hisia chanya na kutokukubali yeyote avuruge utulivu wetu na hisia zetu.
Lakini tunazungukwa na watu ambao maneno yao na hata vitendo vyao vinaweza kuwa dhihaka au matusi kwetu.
Tunapotukanwa au kudharauliwa na wengine, tunapata hasira na hasira hizo zinatutoa kwenye utulivy wetu.
Wastoa wanatufundisha namna ya kuweza kukabiliana na hali hizi ili zisituvuruge. Na zifuatazo ni njia tunazoweza kutumia.
1. Kuwapuuza wale wanaotutukana au kutudhihaki. Kwa kufanya hivi wale waliotutukana watajiona hovyo na kushindwa kuendelea.
2. Kuwachukulia wale waliotutukana kama watoto wadogo, hivyo wanaongea au kufanya vile kwa sababu bado uelewa wao ni mdogo.
3. Tunaweza pia kujifunza kama yule anayetudhihaki au kutukosoa ni mtu mwenye weledi na uelewa mkubwa kwenye kile tunachojifunza.
4. Pia tunaweza kuweka utani kwenye yale matusi ya wengine. Mtu anakutukana halafu wewe unatumia hayo matusi kama utani. Hii inamkosesha nguvu aliyekutukana.
5. Kujifanya kama hujasikia au hujao a kilichotokea, hapa unaendelea na maisha yako kama vile hakuna kilichotokea.
Mbinu hizi tunapaswa kuzitumia kwa akili kulingana na mazingira tuliyopo, ili tusiruhusu watu kututukana na kutudharau tu kama watakavyo wao. Lakini kwa vyovyote vile, usikubali matusi au dharau za wengine zivuruge utulivu wako.
Unamjibuje aliyekutukana?
Tunapotukanwa, ni rahisi kukasirika na kujibu kwa matusi pia.
Lakini wastoa wanatukumbusha kwamba kujibu tusi kwa tusi haitutofautishi sisi na wale waliotutukana.
Hivyo kamwe usirudishe tusi kwa yule aliyekutukana.
Tumia mbinu tulizojifunza hapo juu kuendana na matusi au dhihaka za wengine.