Moja ya mizigo mikubwa ambayo watu wanajijengea wenyewe ni tamaa na kupenda raha. Hivyo watu wengi hukazana sana kuhakikisha kwamba wanapata kila raha wanayotaka.
Lakini mtego unakuja, pale wanapopata raha hiyo, wanakiwa na hofu ya kuipoteza na hivyo wanashindwa kuifurahia raha waliyopata.
Wastoa wanatushirikisha mbinu mbili muhimu za kuweza kuondokana na hali hii.
Mbinu ya kwanza ni KUJINYIMA WEWE MWENYEWE.
Hapa, kwa makusudi kabisa unajinyima kile ulichonacho tayari, kile ambacho unakifurahia lakini una hofu kama kikiondoka utaumia.
Na hapa wastoa wanatuambia tunahitaji kufanya kabisa, na siyo tu kufikiri.
Kwenye mbinu hii unajinyima kile ambacho unauwezo wa kuwa nacho;
Mfano kukaa na njaa kwa muda hata kama chakula kipo.
Kukaa na kiu kwa muda hata kama maji yapo.
Kulala chini hata kama kitanda kipo.
Kuoga maji baridi wakati wa baridi hata kama ya moto yapo.
Na hata kula chakula cha kawaida, au kuvaa mavazi ya kawaida hata kama una uwezo mkubwa.
Kwa kufanya hivi, Seneca anatuambia, tutakuwa tunajiuliza je hiki ndiyo tunachohofia? Na tutaona kumbe tunachohofia siyo kitu cha ajabu, bali tunaweza kuishi nacho.
Mbinu hii ina faida kuu tatu;
1. Inatufanya tufurahie zaidi kile tunachojinyima. Kwa mfano ukiacha kula huku una njaa, utakapokuja kula utafurahia chakula zaidi.
2. Tunaona thamani ya kile tulichojinyima. Mara nyingi tunasahau thamani ya vitu kwa kuwa tumeshavizoea. Kwa kijinyima tunajikumbusha thamani ya vitu hivyo.
3. Tunaweza kujidhibiti na hivyo kuepuka kuendesha na tamaa zetu.
Mbinu ya pili ni kuweza kujidhibiti.
Hapa unajidhibiti ili usiwe mtumwa wa hisia zako.
Unaweza kujiambia kitu fulani hufanyi na hufanyi kweli.
Kwa kuweza kujidhibiti utaweza kujitegemea na kutokujiweka kwenye hali ya kuweza kuyumbishwa.
Muhimu; mbinu ya kujinyima siyo kitu cha kufanya kila wakati, bali unachagua wakati wa kufanya.
Na pia hufanyi kwa sababu unajitesa, bali unafanya kwa sababu unachagua kufanya, unajijengea furaha kupitia kukosa kile ulichozoea kupata.