Kama ambavyo tumeona, falsafa ya ustoa ilikuwa na nguvu kubwa wakati wa utawala wa Roma.
Marcus Aurelius ndiye aliyekuwa mstoa wa mwisho mwenye nguvu.
Marcus pia alikuwa mtawala wa Roma, lakini hakuipandikiza falsafa hii kwa waroma, aliishi yeye kama yeye.
Baada ya Marcus, na kifo cha wastoa kama Epictetus ambao walipenda kuishi na kufundisha falsafa ya ustoa, hapakuwepo na wastoa wa kuendeleza falsafa hii.
Zipo nadharia mbalimbali za kwa nini Ustoa ulianguka.
Mojawapo ni ya kukosekana kwa watu waliojitoa kweli kufundisha na kuishi falsafa hii.
Sababu nyingine ni uongozi mbaya kwenye utawala wa Roma, baada kifo cha Marcus, viongozi waliofuata hawakuwa na maadili na hivyo waroma wengi wakakosa maadili na kushindwa kuishi kwa falsafa.
Sababu nyingine ni kuzaliwa na kukua kwa ukristo, kunatajwa kuchangia sana kufa kwa ustoa. Kwa sababu ustoa na ukrisho unashabihiana kwenye mambo mengi kuhusu maisha na baada ya maisha.
Baada ya anguko hili la Ustoa, wanafalsafa mbalimbali waliendelea kuishi na kuandika kuhusu ustoa. Lakini hapakuwepo na yeyote aliyeufundisha kwa undani.
Katika karne hii ya 21, baadhi ya watu wameanza kuona umuhimu wa falsafa ya ustoa, hasa baada ya kupitia magumu kwenye maisha au kuchoka kukimbiza furaha na wasiipate.
Japo wengi bado wamekuwa na mtazamo hasi kuhusu ustoa, na kuona ni falsafa ya watu wasio na hisia au wanaokandamiza hisia zao.
Kwa namna dunia inavyokwenda, falsafa ya ustoa inazidi kupata umaarufu na inawawezesha wengi kuweza kuwa na maisha bora, yenye furaha muda wote na mafanikio makubwa.