Wastoa wanaelewa kwamba hawawezi kudhibiti kila kitu kinachotokea kwenye maisha yao.
Na kwa vile mambo mengi yanayotokea yanatuathiri moja kwa moja, yana mchango kwenye furaha yetu kwenye maisha.
Hivyo ili kuwa na maisha yenye furaha na yasiyoingiliwa na yale yanayoendelea, wanafalsafa wa ustoa walishauri tuyagawe mambo yanayotokea kwenye makundi mawili, yale ambayo yapo ndani ya udhibiti wetum na hivyo kuweza kuyaathiri na yale ambayo yapo nje ya uthibiti wetu ambayo hatuwezi kuyaathiri.
Kwa yale tunayoweza kuyaathiri, tuchukue hatua na kwa yale tusiyoweza basi tusiruhusu yatusumbue.
Lakini kwenye kuangalia kwa kina mambo yote yanayotokea kwenye maisha yetu, tunaweza kuyagawa katika makundi matatu muhimu.
Kundi la kwanza ni yale mambo ambayo yapo nje ya uwezo wetu kabisa, yaani haya hatuwezi kuyadhibiti kwa namna yoyote ile. Haya ni mambo ambayo hatupaswi kuyaruhusu yatuvuruge, maana hatuwezi kuyabadili.
Mfano wa mambo haya ni kama kuhusu jua kuchomoza kesho, huwezi kuathiri kwa namna yoyote ile, hivyo kuwa na wasiwasi iwapo litachomoza au la, ni kupoteza muda wako.
Kundi la pili ni yale mambo ambayo yapo ndani ya udhibiti wetu kabisa. Yaani tunao uwezo wa kuyadhibiti na kuyaathiri. Tunaweza kuyabadili kadiri tunavyotaka sisi wenyewe. Haya ndiyo mambo tunayopaswa kuchukua hatua mara moja.
Mfano wa mambo haya ni maoni yetu binafsi juu ya mambo, malengo tunayojiwekea na hata hisia zetu.
Kundi la tatu ni yale mambo ambayo tunaweza kuyadhibiti kwa kiasi. Yaani hatuwezi kuyadhibiti au kuyaathiri kabisa, bali tuna sehemu ambayo tunaweza kuiathiri.
Mambo haya ndiyo yana changamoto kubwa kwa sababu wengi huwa hayujui udhibiti wetu unaishia wapi, na hivyo kujikita tukiumia kwa jambo ambalo halikuwa ndani ya uwezo wetu.
Kwenye mambo haya, tunapwswa kujua mwisho wa udhibiti wetu ni wapi, na kuchukua hatua sahihi.
Mfano wa mambo haya ni kushinda mchezo wa tenesi, unaweza kuwa na malengo mazuri ya kushinda, lakini hilo halipo ndani ya udhibiti wako kabisa, kuna mengi yanaweza kutokea yakafanya usishinde, na kuwezi kuyadhibiti. Hivyo kwenye hali kama hii, unachopaswa kufanya ni kufanya ile sehemu yako, kujiandaa kwa kadiri ya uwezo wako, kufanya kila lililopo ndani ya uwezo wako, lakini kutokuweka kwamba lazima ushinde.
Kwa maandalizi hayo ukishinda ni sawa na hata ukishindwa hutaumia kwa sababu unajua umeweka juhudi zako zote.
Utatu huu wa udhibiti ni msingi muhimu kwenye maisha yetu hasa kwenye mambo tunayokutana nayo kwenye maisha yetu ya kila siku.