Vijana huwa wanaona dunia kama ni mali yao.
Huona wana uwezo wa kufanya chochote wanachotaka kufanya na hawaoni umuhimu wa kuwa na maisha ya utulivu.
Ni vigumu sana kumshawishi kijana kuielewa falsafa ya Ustoa kwa sababu anaona ana kila kitu.

Lakini kijana anapofikia utu uzima, anapoanza kukosa kile anachotaka, ndiyo anagundua kwamba maisha siyo rahisi kama alivyokuwa akifikiria. Inambidi kufanya kazi sana ili kupata kile anachotaka. Anakazana kweli na kupata, lakini mara nyingi anajikuta hana furaha.
Anagundua kwamba alichokuwa anafanyia kazi siyo hasa alichotaka. Na hapa ndipo maisha ya wengi huvurugika.

Baada ya utu uzima, unakuja uzee, hapa ndipo mtu anapojua kwa hakika ya kwamba atakufa. Anapoteza uwezo wa kimwili aliokuwa nao kwenye maisha yake na kujua anachosubiri ni kifo pekee.
Wengi huruhusu hali ya uzee kuwaletea msongo au sonona na kujikuta wakiwa hawana furaha na hii kupelekea kufa haraka zaidi.

Falsafa ya ustoa ni falsafa bora sana kwa wakati wa uzee.
Kwani kwa kuwa mstoa, unakuwa na utulivu na furaha muda wote.

Seneca anasema badala ya kusikitika kwamba uzee unapunguza uwezo wetu kimwili, tufurahie kwamba uzee unaondoa tamaa zetu na hivyo kutuweka huru zaidi.
Unapokuwa mzee vitu kama tamaa za vyakula, mapenzi havina nguvu tena kwako na hivyo huwezi kuwa mtumwa wa tamaa zako.

Pia anatuambia wakati wa uzee ndiyo wakati wa kujali zaidi muda wetu.
Mtu mwenye miaka 20 anaweza kuchukulia muda kirahisi kwa sababu anaona anao mwingi sana.
Lakini mwenye miaka 80 atauchukulia muda kwa uzito wake, kwa sababu anajua atakufa siku siyo nyingi, hivyo kuiona leo ni bahati ya kipekee.

Hivyo badala ya kuhofia uzee na kuchukulia kama ni sehemu mbaya ya maisha yetu, tuupokee kwa furaha na kuufaidi.