Habari za asubuhi ya leo rafiki,
Ni siku nyingine nzuri sana ya leo, ambapo tumepata nafasi ya kipekee kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

img-20161217-wa0002
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NGUMU NA ADIMU…
Vitu vigumu na vitu adimu ndiyo vitu ambavyo watu wanavipa thamani zaidi.
Kama kitu ni rahisi watu wanakichukulia poa, hawakipi uzito na wanaona ni rahisi kufanya. Lakini kinapokuwa kigumu watu wanakiheshimu, wakijua ni kigumu na hawawezi kufanya.

Kitu kisipokuwa ADIMU watu wanakidharau, wanajua wanaweza kukipata muda wowote wanaokitaka, hivyo hawajisumbui kuhangaika kukipata. Lakini kinapokuwa adimu watu wanakithamini sana, wanaweka juhudi kubwa ili kuhakikisha wanakipata, na wanapokiona, hawakidharau hata kidogo, maana wanajua kukiona tena ni shida.

Hili linafaa kwa kila kitu kwenye maisha, na hata kwa watu pia.
Hivyo hata wewe ukiwa MGUMU KUPATIKANA na ukawa ADIMU KUONEKANA, watu wanaheshimu uwepo wako na kutumia vizuri uwepo wako.
Lakini ukiwa rahisi kupatikana na kupatikana popote, watu wanadharau uwepo wako na wanakupotezea muda wako, kwa sababu wanajua upo tu na muda wowote watakupata.

Anza kuongeza thamani yako kwa kuweka ugumu kwenge upatikanaji wako na uadimu kwenye muda wako. Na waka huhitaji kuigiza hili, wewe anza tu kufuatilia yale muhimu kwako, kuwa na vipaumbele vya maisha yako na tumia vizuri muda wako, watu wataanza kuona uadimu wake na kuheshimu uwepo wako, popote pale.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.