Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu,
Hongera kwa siku hii nzuri sana ya leo.

img-20161217-wa0002
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa sana.
Ni kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutawexa kufanya makubwa.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUJIFUNZA KUUZA….
Kama kuna kitu kimoja ambacho kila mtu hapa duniani anapaswa kujifunza basi ni kuuza.
Kwenye maisha kila kitu ni kuuza, kama huwezi kuuza huwezi kupata chochote unachotaka.

Unaweza kuwa na bidhaa au huduma nzuri sana, lakini kama huwezi kuuza, kama huwezi kuwashawishi watu wanunue kwako, hutaweza kupata wateja.

Unaweza kuwa na utaalamu bora na wa kipekee kabisa, ambao unapaswa kulipwa zaidi kwa yale makubwa unayofanya, lakini kama huwezi kuuza huo utaalamu wako kwa watu sahihi, utabaki unaumia.

Unaweza kuwa mwandishi mzuri sana, lakini kama huwezi kuuza ulichoandika, kama huwezi kushawishi watu wasome na kununua, hutapata wasomaji wa kazi zako.

Pia unaweza kuwa na mawazo mzuri sana ya kimaendeleo, unaweza kuwa na mbinu bora za watu kupiga hatua, lakini kama huwezi kuuza mawazo hayo kwa wale ambao yanawahusu, huwezi kupata ushawishi.

Kama tunavyoona, kila kitu kwenye maisha yetu ni kuuza, hivyo kadiri unavyokuwa bora kwenye kuuza, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kupata kile unachotaka.

Jifunze kuuza, kila siku, zijue mbinu mbalimbali za ushawishi ili kuwafanya watu wajue na waje kwenye kile unachofanya. Na wakishafika wape kilichobora, ili waendelee kuja zaidi na zaidi.

JIFUNZE KUUZA, ITAKUSAIDIA SANA KUFANIKIWA.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.