Msingi wetu mkuu tunaouishi kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA. Hizi ni nguzo tatu muhimu sana kwenye mafanikio ya maisha yetu, kuanzia kwenye kazi, biashara, mahusiano, afya na kila eneo la maisha yetu.

IMG-20170314-WA0016

Uadilifu unaendana sana na uaminifu, japo siyo kitu kimoja. Uaminifu ni kile unachosema na kufanya, uadilifu ni vile unavyoishi, kutokana na uaminifu wako. Hivyo uaminifu na uadilifu vinakwenda pamoja sana. Zote ni tabia za mafanikio.

Lakini tunaishi kwenye dunia ambavyo uaminifu imekuwa bidhaa adimu sana. Tunaishi kwenye ulimwengu ambao kila mtu yupo tayari kufanya lolote, ili mradi tu apate kile anachotaka kupata, hata kama kwa kufanya hivyo anawaumiza wengine. Na kwa njia hii anaweza kupata, lakini wote tunajua hadithi zao huwa zinaishiaje. Wote tunajua wale wanaopata utajiri kwa njia ambazo siyo halali namna ambavyo huja kusumbuka baadaye. Unaweza kuipata fedha kwa wizi au ufisadi, lakini ukatumia maisha yako yote kupambana na kesi, au kujaribu kujisafisha na usitakate.

SOMA; Umuhimu Na Jinsi Ya Kujenga Uaminifu Kwa Wateja Wako.

Wapo watu wamemezwa kabisa na aina hii ya maisha mpaka wanadiriki kusema ukiwa mwaminifu huwezi kufanikiwa, hasa kwenye swala la fedha. Watu watakuambia kabisa matajiri wana namna ambazo wanafanya mpaka wamefika pale. Lakini huo siyo ukweli, ukweli ni kwamba, mafanikio ya kweli, na yanayodumu, ni yale ambayo yamepatikana kwa njia ambazo ni halali. Yale ambayo yamepatikana kwa uaminifu.

Hivyo, tunakubaliana kabisa ya kwamba, lazima tuwe waaminifu. Kama hukubali hili, nikuambie tu kwamba, mafanikio kwako yatakuwa ndoto, hata kama utayapata, yatakuponyoka haraka sana, au yatakuwa mzigo mzito kwako kuubeba.

Sawa, uaminifu ni muhimu, lakini tunawezaje kuwa waaminifu, hasa kwa vile tunaishi kwenye mazingira ambayo uaminifu ni adimu? Hapa nakwenda kukushirikisha mambo ya kufanya ili kujijengea uaminifu.

Lakini kabla sijakuambia mambo haya, naomba nikuombe jambo moja muhimu, ukishachagua kuwa mwaminifu, basi kaa mbali sana na wale ambao siyo waaminifu. Kaa mbali pia na wale wanaokuambia ukiwa mwaminifu huwezi kufanikiwa. Watu hawa ni sumu, watachafua mawazo yako na kukufanya ushindwe kupiga hatua.

Kama tumeshakubaliana kwenye hilo, basi hata ndiyo mambo ya kufanya ili kujijengea uaminifu kwenye maisha yako na uweze kufanikiwa.

  1. Usiwe na maisha ya aina mbili.

Kuna watu wana maisha ya aina mbili, au hata zaidi. Kuna namna ambavyo anaonekana na tabia anazokuwa nazo akiwa eneo moja, halafu akienda kwenye eneo jingine kuna mwonekano na tabia nyingine. Kwanza hapa unajidanganya wewe mwenyewe, na wale ambao watakugundua aina yako hiyo ya maisha, basi hawatakuamini.

Umeshawahi kusikia au kuona mtu amemjibu vibaya mtu ambaye hamjui, baadaye anakuja kukuta labda yule mtu ni ndugu yake au anahitaji msaada wake. Halafu anamwambia sikujua kama ni wewe? Hii inaonesha namna ambavyo watu wanaishi maisha ya aina tofauti. Kwamba kama ni mtu unamjua basi utamheshimu, kama humjui utamdharau! Sasa unajua utakuwa unaangukia upande upi? Upande wa watu wasiokuwa na heshima.

Kama umechagua kuwa na heshima, kama ndiyo unataka kuonekana kwa wengine, basi popote ulipo, kuwa na heshima. Mheshimu kila mtu, hata kama humjui, hata kama ni mdogo kwako, kiumri au kicheo.

Hakuna wakati mbaya wa kuwa na maisha ya aina mbili kama sasa. Nimekuwa nawaambia watu sasa hivi hakuna siri tena, kila kitu unachofanya kuna watu wanakurekodi, amini hilo. Hivyo wewe unaweza kuongea na simu na mtu, ukijua ni yeye tu unaongea naye, ukaongea utakavyo, kumbe mwenzako anarekodi na anaweza kuweka wazi yale uliyoongea. Hata popote unapopita, hata kama ni mafichoni, yupo ambaye anaweza kukupiga picha bila hata ya wewe mwenyewe kujua.

Njia pekee ya kupona nyakati hizi, na kulinda heshima na jina lako, ni kuwa na maisha mamoja na kuyaishi hayo, popote unapokuwa, hata kama ni mafichoni.

SOMA; Biashara ni uaminifu na sio pata potea.

  1. Fanya kile ambacho umesema utafanya.

Karibu kila mtu anadanganya siku hizi. Anayeajiri anadanganya kuhusu maslahi atakayompa mwajiriwa, anayeajiriwa anadanganya kuhusu kiwango cha kazi atakachofanya, au sifa alizonazo. Anayeuza anamdanganya mteja kuhusu kile anachopata akinunua. Kwa hali hii, watu wamekuwa hawaamini tena kile wanachoambiwa, bali wanaangalia kile kinachofanyika. Hivyo piga kelele utakavyo, jisifie utakavyo, watu hawataweka uzito kwenye maneno yako, badala yake wataangalia unachofanya. Na hicho ndiyo watakachokichukua.

Hivyo, kupona zama hizi, fanya kile ulichoahidi, na mara zote, angalia fursa ya kupitiliza zaidi. Weka juhudi kubwa na hakikisha unatimiza ulichoahidi.

  1. Usitoe sababu, tafuta namna ya kufanya.

Ukiwa mtu wa sababu sana, hata kama ni za kweli, watu wanakuchukulia ni ‘wale wale’. Sasa rafiki yangu, ogopa sana neno wale wale, mtu akishakuambia wewe ni wale wale, maana yake haoni tena thamani kwako, hakusikilizi tena, kwa sababu hakuna cha tofauti unachoweza kufanya.

Unaposhindwa kutimiza chochote ulichoahidi, hata kama ni kwa sababu ambazo zimekushinda kabisa, usijitetee kwa sababu hizo, bali waambie watu utafanya nini. Tena hata usipoteze muda kuwaambia utafanya nini, badala yake fanya huo mbadala na kisha waambie kwa kula ulichoahidi kimeshindikana, umefanya hichi ambacho kitawasaidia pia.

Usiwe mtu wa sababu, angalia nini unaweza kufanya.

  1. Usishiriki umbea au majungu.

Lolote baya utakalosema kuhusu mtu, litamfikia, hata kama ni siri kiasi gani. Taarifa zitamfikia kwamba ulisema hichi na kile kuhusu yeye. Na mbaya zaidi uliyosema yatakuzwa kuliko hata ulivyosema wewe, lakini sasa, hutakuwa na nana ya kujitetea, maana ulisema.

Hii inatukumbusha kwamba tusishiriki umbea au majungu ya namna yoyote ile. Mtu yeyote anayekuletea habari za umbea na majungu kuhusu wengine, mkatishe haraka sana na usikubali kuwa msikilizaji. Maana unaweza kusikiliza, na ukajikuta umeongea neno kwa mema tu, lakini likatafsiriwa vibaya na wewe ukawa umejumuishwa kwenye umbea huo.

Kama ni watu ambao wako chini yako wanakuletea taarifa za aina hii, unahitaji kuwaleta pamoja wote wanao toleana taarifa ambazo huenda ni majungu au umbeya, na kila mtu aongee mwenzake akiwa anasikia. Kusikiliza mmoja mmoja unaweza kujikuta unachanganywa na majungu yanayoendelea.

  1. Beba lawama.

Kuna wakati ambapo watu wanaweza kukubebesha wewe lawama ambazo hata hustahili. Lakini kukazana kukataa lawama hizo kunazidi kuwafanya watu wakuchimbe na kukusumbua zaidi. Nyakati kama hizi unaweza tu kukubali kubeba lawama na kuahidi kuchukua hatua. Utafika wakati watu wataujua ukweli na watakuheshimu sana kwa hatua ulizochukua.

Hasira zinaficha hofu, hasira zinapunguza uwezo wa kufikiri na hasira zinaweza kupelekea ukafanya maamuzi ambayo baadaye utayajutia. Usikubali hasira zikutawale, na jizoeshe kutokupata hasira. Utakuwa umepata ushindi mkubwa sana kwenye maisha yako.

  1. Sema kile unachotaka kusema, ila usiumize wengine.

Hapa ndipo pagumu zaidi na ndipo wengi husema wengine ni wanafiki na wao siyo wanafiki. Kuna wakati mtu anakuwa na kitu anataka kusema, anaamini ni sahihi kabisa kwake kusema, lakini anachagua kutokusema kwa sababu labda hataki aonekane yeye ndiyo yupo kinyume. Unaweza kuficha hivi lakini baadaye watu wakija kugundua ulikuwa unasimama wapi na hukuonesha msimamo wako wakati huo, watakuona siyo mwaminifu na hawatakuheshimu.

Hivyo mara zote, sema kile ambacho unataka kusema, lakini unapokisema, usiwaumize watu. Hata kama ni jambo la kuumiza, liseme kwa njia ambayo itamsaidia mtu kujenga zaidi na siyo kumbomoa. Sema kile unachoamini ni sahihi, na utajulikana unasimamia wapi na watu watanufaika pia na kile unachosimamia.

Uaminifu ni bidhaa adimu kwenye zama hizi tunazoishi, jijengee uaminifu na huu utakuwa mtaji mzuri kwako kuweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako. Fanyia kazi haya ambayo umejifunza, hutabobea kwenye mambo yote ndani ya siku moja, bali utaendelea kujifunza kadiri siku zinavyokwenda. Muhimu ni wewe kupiga hatua kila siku ili kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog