Hongera kwa siku ya leo rafiki yangu,
Najua yapo mengi umejifunza na zipo changamoto umekutana nazo.
Hakikisha kila ulichopitia leo, kinakuwa somo kwako hapo kesho, ili uwe bora zaidi.
Karibu kwenye #GHAHAWA leo tuangalie namna tunavyokosea kufikiri na hatimaye kufanya maamuzi.
Hadithi za watu waliofanikiwa zipo kila mahali,
Hadithi za walioshinda zipo kila mahali,
Na hivyo tunapotaka kuanza kufanya kitu, tunaangalia hawa walioshinda na kufanikiwa.
Lakini tunachosahau ni kwamba, katika wachache waliofanikiwa, wapo wengi ambao walianza nao, lakini wameshindwa.
Tatizo ni kwamba, hadithi za walioshindwa hazivutii, hivyo haziandikwi na kufuatiliwa na wengi.
Wale wanaopona ndiyo wanaoandika, wanaokufa hatupati fursa ya kujifunza kutoka kwao.
Wengi tumekuwa tunachukua hadithi hizi za wachache, na kuchukua kama mfano, tunafanya kila walichofanya lakini tunashindwa.
Ili kuepuka kurudia makosa haya, ni muhimu kabla hatujakubaliana kirahisi na hadithi za waliofanikiwa, tuangalie na wale walioshindwa pia. Tuangalie wakati hawa waliofanikiwa wanaanza, wale walioanza nao wako wapi? Na hapo tutajifunza mengi zaidi na kujua kama kweli mafanikio yao yametokana na kile kinachoonekana kwa nje na kuandikwa, au kuna mengine mengi yasiyoonekana ambayo yamechangia kufanikiwa kwao au kushindwa kwa wengine.
Hufanyi hivyi ili kukata tamaa, bali upate uhalisia wa kazi iliyopo mbele yako.
Nikutakie usiku mwema rafiki yangu,
Kama una lolote la kuchangia kuhusu #GHAHAWA ya leo karibu sana.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.
http://www.amkamtanzania.com
