Kama wapo watu tofauti, ambao wanafanya kitu kimoja, na kati yao wachache wakawa wanafanya vizuri kuliko wengine, ni dhahiri kuna tofauti kati yao katika utendaji. Hata kama wanaonekana wanafanya kwa usawa kabisa, ukichunguza kwa ndani, utaona zipo tofauti, hata kwa kuanzia kwenye tabia na mtazamo ambao watu hao wanao katika ufanyaji wa mambo yao.
Leo tunakwenda kuangalia tabia adimu za kijasiriamali, hizi ni tabia ambazo utazikuta kwa wajasiriamali wenye mafanikio makubwa lakini hazipo kwa wengine. Hizi siyo zile tabia za kawaida, za kujituma, kutokata tamaa na kuwa na mtazamo chanya wa mafanikio. Ni tabia ndogo ndogo ambazo zinawapa upenyo wa kusonga mbele ukilinganisha na wengine ambao wanabaki nyuma.
Kutokukomaa sehemu moja.
Japokuwa wajasiriamali wenye mafanikio ni ving’ang’anizi na wavumilivu, hakuna kitu wanakijua vizuri kama sumu inayomaliza wengi, ambayo ni kukomaa sehemu moja. Wapo watu ambao wanaanzisha biashara, inakuwa na mafanikio halafu wanajisahau kabisa. Kila siku wanafanya vile vile walivyozoea kufanya. Miaka inaenda wao wapo pale pale. Sasa kama unavyoijua sheria ya dunia, kila kitu kinabadilika, isipokuwa mabadiliko yenyewe. Hivyo mabadiliko yanapokuja, wale wanaofanya kwa mazoea huachwa nyuma.
SOMA; Makosa Makubwa Yanayofanywa Na Wajasiriamali Wageni.
Wajasiriamali wenye mafanikio, mara zote wapo mbele ya mchezo wao. Utawaona sasa wapo kwenye biashara hii, lakini sipo mawazo yao yote yalipo, wanazidi kuangalia mbele, wanazidi kufikiria namna gani wataboresha zaidi kile wanachofanya. Wanazidi kuangalia namna gani mambo yanabadilika. Kwa njia hii, wanakuwa wa kwanza kuchukua hatua pale mambo yanapobadilika.
SOMO; hata kama biashara yako kwa sasa ni kubwa na inalipa kiasi gani, usijisahau na kufanya kwa mazoea. Mambo yanabadilika, kuwa macho muda wote na angalia fursa nyingi zaidi.
Kutokuhofia kupoteza kiasi cha uwekezaji wao.
Ni jambo moja kusema kupoteza ni sehemu ya biashara, na jambo jingine kabisa pale unapopoteza hasa. Kupoteza kunaumiza, kupoteza kunahatarisha, na hakuna anayependa kupoteza hata kidogo. Hivyo kwa tabia zetu sisi binadamu, panapokuwa na dalili za kupoteza, huwa tunasita kuchukua hatua. Na hii ndiyo inapelekea watu wanafanya kile ambacho wamezoea kufanya, kwa sababu tayari wana uhakika hawawezi kupoteza.
Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa, wanajua kupoteza ni sehemu ya kupata. Hivyo katika kujaribu kwao mambo mapya, katika kuongeza kwao ubunifu, wanapoteza kiasi, lakini wanajifunza na kupata njia bora zaidi za kulipa kile ambacho wamepoteza.
Kama hutaki kupoteza kabisa, na unachotaka wewe ni kupata tu, utapata kidogo na mwishowe utapotea kabisa. Kwa sababu mabadiliko yatakapokuja, yanakupoteza wewe kabisa.
SOMO; Kuwa tayari kupoteza sehemu ua uwekezaji wako, pale unapojaribu mambo mapya. Bila ya utayari huu utaendelea kufanya yale uliyozoea kufanya na huwezi kupiga hatua.
Kutokuwa na aibu au kuogopa kudhalilishwa.
Kama una aibu, hasa kwa watu, ni njia ya haraka sana kushindwa kwenye biashara. Kwa sababu biashara inakutaka uwe wazi mbele ya watu. Wapo watu watakushambulia hata kama hakuna jambo baya umefanya. Wapo watu watakuchukia tu kwa mafanikio yako. Wapo watakaokuja na hadithi zinazoonekana kama za kweli kabisa. Na hata unapofanya jambo sahihi, wapo watakaolichambua kama siyo sahihi.
Wajasiriamali wenye mafanikio wanalijua hili na wanapambana kuhakikisha wanapata kile wanachotaka. Hawaoni aibu kusimamia kile wanachojua ni sahihi. Hawaogopi wale wanaowadhalilisha kwa sababu wanajua ni kwa muda tu. Ukweli wote utakuwa hadharani muda siyo mrefu na wao wataendelea kusimama.
SOMO; Kwenye biashara na ujasiriamali, usione aibu, usitake kuonekana mwema wakati wote. Badala yake fanya kile ambacho ni sahihi, kisimamie hata kama kila mtu anakipinga. Uzuri wa ukweli huwa haupotei, ni swala la muda pekee.
Huteleza mara nyingi, lakini hawakubali kuanguka.
Kuna kuteleza na kuanguka kwenye ujasiriamali. Kuteleza kupo kwa aina nyingi, na kunasababishwa na mengi. Lakini kuanguka ni kitu kimoja tu, pale unapokata tamaa na kuacha kile unachofanya. Hapo ndipo unakuwa umeanguka na unakuwa umechagua wewe mwenyewe.
SOMA; Mambo matano(5) muhimu ambayo hujawahi kuambiwa kuhusu ujasiriamali.
Wajasiriamali wenye mafanikio huchukulia kila wanachopitia kama utelezi, wamepata hasara, mambo magumu, wamefilisika, yote hayo kwao ni utelezi. Wanachokazana ni wasianguke, wasifike mahali na kusema sasa siwezi tena. Kwa kuepuka hili, wamekuwa wanaendelea kudumu na hata kufanikiwa licha ya kupitia magumu.
SOMO; usikubali kuanguka, lolote unalopitia jua huo ni utelezi, kiama ni kuchagua mwenyewe kuanguka.
Hawakai nje ya mchezo kwa muda mrefu.
Kuna wakati utelezi huwa mkubwa na kuwafanya wajasiriamali kukaa nje ya mchezo kidogo ili kuusoma mchezo. Hapa kuna tofauti kubwa kwa wajasiriamali wanaofikia mafanikio makubwa na wanaoshindwa. Wajasiriamali wanaofanikiwa, hawakai nje ya mchezo kwa muda mrefu, wanahitaji muda mfupi sana wa kujipanga upya na huanza haraka, hata kama hawana kitu kabisa, wanaanzia popote wanapoweza kuanzia. Haiwachukui muda wanakuwa wamesharudi tena kwenye mchezo na mambo yanakwenda vizuri.
Wajasiriamali wanaoshindwa, wanapoteleza hukaa nje ya mchezo kwa muda mrefu. Kila wanapotaka kuanza hujikumbusha namna walivyoteleza na kujiona bado hawajawa tayari, bado kuna kitu wanakosa na hivyo kuendelea kusubiri. Kadiri wanavyosubiri, ndivyo inavyozidi kuwa vigumu kwao kurudi tena kwenye mchezo.
SOMO; unapoteleza, unaweza kukaa chini na kujitathmini wapi umekosea na kujipanga kuanza tena. Lakini ukichukua muda mrefu kwenye hilo, unahama kwenye kuteleza na unajikuta umeshaanguka. Hata kama huna pa kuanzia, anzia popote. Ni rahisi unapokuwa kwenye mchezo kuliko ukiwa nje ya mchezo.
Hizo ndizo tabia zinazowatofautisha wajasiriamali wenye mafanikio na wale wanaoishia kuwa wa kawaida. Kama ulivyoona, siyo tabia ambazo ni maarufu kwa wengi, lakini zinawapa watu faida kadiri wanavyokuwa nazo kila siku. Ongeza tabia hizi kwako utaweza kupiga hatua kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
