Habari rafiki kwa kuimaliza siku hii nzuri ya leo.
Nina hakika yapo mengi umeshinda leo, na pia yapo ambayo umejifunza, ambayo wengi wanasema wameshindwa. Ila wewe hujashindwa, umejifunza na kesho utafanya kwa ubora zaidi.

Karibu kwenye #GHAHAWA jioni ya leo, ambapo tunakwenda kuangalia makosa ambayo tumekuwa tunafanya kwenye kufikiri.
Akili zetu zina uwezo wa kipekee sana, zina uwezo wa kutengeneza chochote, hata ambacho hakipo kabisa.
Wengi wamekuwa wanatumia nguvu hii kutengeneza hofu, na wapo ambao wamekuwa wanaitumia kutengeneza mafanikio.
Kujua nguvu hii ya akili zetu, je umewahi kuangalia angani na kuona mawingu yametengeneza picha fulani? Labda kama sura ya mtu? Au kitu ambacho kinajulikana?
Je umewahi kuangalia kwenye mwezi na kuona picha ya mwanamke amebeba kuni na mtoto mgongoni? 😄😄
Hivi ni vitu ambavyo watu wamekuwa wanaona, lakini havijawahi kudhibitishwa iwapo vipo.
Kama ambavyo ukiwa na hofu na kuingia kwenye chumba chenye giza, unaweza kuona vitu vya kutisha, lakini ukiwasha taa havipo.
Hizi ni picha ambazo akili zetu zinatengeneza, na tunaziona kweli. Na mara nyingi utaambiwa huoni kabisa kile ni kitu fulani? Na ghafla unaanza kukiona, wakati dakika chache ulikuwa unaona.
Hii ni nguvu ya akili katika kutengeneza picha ya kile unachofikiri.
Hali hii imekuwa inawafanya watu kuamini vitu ambavyo havipo.
Lakini pia tunaweza kuitumia vizuri kutengeneza kile ambacho tunataka na kufanyia kazi.
Kila tunapojaribu kutengeneza picha kutokana na fikra zetu, ni vyema kufikiri kwa kina kama kitu kipo kweli au tunatengeneza kwa akili zetu.
Nakutakia maandalizi mema ya kesho.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.