Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Nina imani kubwa yapo makubwa uliyofanya leo, na pia yapo mengi uliyojifunza. Nikukumbushe kutosahau chochote ulichojifunza.

Kwenye #GHAHAWA yetu ya leo tunakwenda kuangalia namna tunavyoponzwa na kundi kubwa, kufanya kitu ambacho siyo sahihi.
Kwa mfano umetoka nyumbani na unakwenda kwenye tamasha fulani, njiani ukakutana na kundi la watu wanaangalia kitu angani, wewe unafanyaje? Moja kwa moja unaangalia angani…
Unafika kwenye tamasha, wakati tamasha linaendelea, mtu mmoja anaibuka na kuanza kupiga makofi, watu wanapokea na wewe unafanya nini? Unapiga makofi….
Sasa unaweza kusema kwa nini uliangalia juu, wakati hukuwa na mpango wala sababu yoyote? Au kwa nini ulipiga makofi? Ulifanya kwa sababu wengi wanafanya.
Na akili zetu huwa zinarubuniwa na hata kujirubuni sisi wenyewe, pale ambapo jambo linafanywa na kila mtu, tunaona siyo vibaya na sisi tukifanya, hata kama ni jambo ambalo halina maana yoyote kwetu.
Hali hii ilikuwa na msaada kwa wazee wetu waliopita kale sana. Kama walikuwa msituni kuwinda, halafu mmoja ghafla akaanza kukimbia, ilikuwa ni bora kuwafuata wanaokimbia, la sivyo unaweza kuliwa na simba au chui. Na kama siyo chui au simba kweli, hakuna unachokuwa umepoteza. Ila ungesubiri, na akawa simba kweli, basi ungeliwa.
Hali imebadilika sana sasa, lakini bado hatujabadili hili.
Tunaamini sana kwenye wengi na siyo kwenye usahihi.
Matangazo ya biashara huwa yanatumia hii kutuhadaa, kutuonesha kwamba bidhaa fulani ndiyo inakubalika na wengi, na sisi tunaamini wengi wapo sahihi.
Epuka kufikiri kwa njia hii, anza kuangalia na kuhoji kila kitu. Mara nyingi kitu kinachofuatwa au kukubaliwa na wengi, siyo kitu sahihi.
Kama watu milioni 50 wanakubaliana na kitu, kama siyo sahihi, kitabaki kuwa siyo sahihi. Wingi wa watu haubadili chochote. Mara zote kazana kuwa upande sahihi na siyo upande wa wengi.
Uwe na mapumziko mema rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
Contacts; makirita@kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.