Maisha ya mafanikio hayaji kwa kubahatisha. Maisha ya mafanikio ni matokeo ya kujifunza maarifa tofauti tofauti ambayo mwisho wa siku maarifa hayo huweza kutusaidia kufikia mafanikio ambayo tunayategemea.
Kama maisha ya mafanikio hayaji kwa kubahatisha na msingi wake upo kwenye maarifa, tafsiri yake ni kwamba unalazimika kila wakati kujua maarifa ya msingi ambayo yana uwezo mkubwa wa kukupeleka kwenye mafanikio yako.
Kwa kusoma makala haya utajifunza maarifa ya msingi ambayo yana msaada mkubwa wa kukupeleka kwenye mafanikio moja kwa moja. Maarifa hayo ya msingi ni yapi? wala usitie shaka sasa twende pamoja tuweze kujifunza.
1. Kufanya kazi kwa juhudi.
Mafanikio yote yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa. Hivyo ni vyema kuelewa kujua ile dhana ya kufanya kazi kwa bidii kubwa ndio kitu ambacho kitakupeleka kwenye mafanikio makubwa na sio kitu kingine kile. Haya ni maarifa ya msingi sana kwako ambayo unatakiwa uyafanyie kazi vya kutosha hadi kufanikiwa.
2. Kuwajibika.
Hakuna mtu ambaye unatakiwa umlaumu katika maisha yako zaidi yako wewe. Unatakiwa kuwajibika katika maisha katika kila kitu. Unatakiwa kuwajibika juu ya uchumi wako na kila kitu ambacho wewe binafsi unakitawala kwenye maisha yako pia. Bila ya wewe kujifunza misingi ya kuwajibika utaishia kulaumu tu katika maisha yako.
3. Kutatua changamoto.
Maarifa mengine ambayo unatakiwa uyaelewe na kuyafanyia kazi ni juu ya kutatua changamoto. Kila wakati unatakiwa ujifunze kutokimbia changamoto. Unatakiwa uwe mtu wa kutatua changamto hata ije ngumu na nyingi vipi, maarifa hayo unatakiwa uwe nayo ili uweze kujenga mafanikio yako, kwani kwenye changamoto ndipo mafanikio yalipo.
4. Kupanga na kufanikisha malengo.
Katika maisha haina maana kuishi tu na kusahau suala zima la kupanga na kufanikisha malengo. Ni lazima ujue unapopanga kitu pia  ni lazima kukitimiza. Hata ikitokea changamoto ni nyingi ni vyema ukaweza kuzitatua changamoto hizo na kuhakikisha mpaka unaweza kutimiza malengo yako.
5. Ushirikiano.
Mafanikio pia yanapatikana kwa ushirikiano kati ya mtu mmoja na mtu mwingine. Katika maisha yako ili uweze kufikia kilele cha mafanikio unalazimika sana kuwa na ushirikianao na wengine ambao ni mzuri. Unaposhirikiana na wengine inakuwa ni njia sahihi ya kuweza kukufanikisha kwa wepesi sana.
6. Ung’ang’anizi.
Maarifa mengine ambayo unatakiwa ujifunze na kuyaelewa vizuri ni kujua  namna ya kuwa king’ang’anizi katika maisha. Unapokuwa king’ang’anizi unakuwa ni mtu ambaye hukubali kushindwa kwa namna yoyote ile mpaka yale malengo yako yote ya msingi yatakapoweza kutimia.
 7. Uvumilivu.
Kati ya kitu ambacho kina msaada mkubwa katika kuyafikia mafanikio yako ni kwa wewe kujenga moyo wa uvumilivu. Tunapitia changamoto nyingi, hivyo ni vyema kuweza kujenga uvumilivu wa kutosha, vinginevyo ni ngumu sana kuweza kufanikiwa kama huo uvumilivu hautakuwepo.
8. Mahusiano bora.
Si mbaya sana kama pia ukajifunza namna unavyoweza kujenga mahusiano na wengine yatakayoweza kukusaidia kufnaikiwa. Jitahidi sana jenga mahusiano bora ya kibiashara. Pia jenga mahusiano hata ya kawaida ila yawe bora. Kumbuka fursa hazitoki hewani, hivyo ni vyema kuwa na mahusiano sahihi yatakayo kusaidia kufanikiwa.
9. Udadisi.
Katika maisha acha kujizoeza kukubali kila kitu. Hebu kuwa na udadisi na mambo mengi. Kila wakati dadaisi kwa nini hiki kiko vile na kwa nini kile kipo vile. Kila unachoambiwa jihoji kwanza kwamba je, huo ndio uhalisia wake? Ukifanya hivyo itakusaidia sana kuweza kuishi kwa kutokijiingiza katika makosa ambayo hukutakiwa kufanya.
10. Maamuzi sahihi.
Pia ni vyema na inapendeza ikiwa utajifunza maarifa ya kuwa na maauuzi sahihi. Unapokuwa na maamuzi sahihi inakusaidia kuweza kutimiza ndoto na mipango yako kwa urahisi sana. Watu wenye mafanikio kila wakati wana jitahidi kufanya maamuzi sahihi yatakayosaidia kuweza kufika kwenye ndoto zao.
Hayo ndiyo maarifa ya msingi ambayo unatakiwa ujifunze na kuyafanyia kazi karibu kila siku katika maisha yako. Fanyia kazi na chukua hatua.
Kwa makala nyingine za mafanikio tembelea DIRA YA MAFANIKIO kuweza kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,