Umewahi kununua kitu, halafu baadaye ukajikuta unajutia kununua kitu kile? Wakati unanunua ulijishawishi kabisa ya kwamba unakihitaji na umepata kwa unafuu, lakini baada ya kukinunua wala hujawahi kukitumia! Au umekitumia mara chache mno?
Hali hii ipo sana kwenye vitu vidogo vidogo kama mavazi, pia tabia hii inawaathiri zaidi wanawake.
Swali jingine; umewahi kuwa na fedha ukajikuta umezitumia kwa mambo ambayo hukuwa umeyapangilia? Au kabla ya fedha unakuwa na mipango mizuri, lakini ukishakuwa nazo unashangaa mambo mengine yanayoonekana muhimu zaidi yanajitokeza na kumaliza fedha ile?
Hili pia limekuwa linasumbua wengi mpaka wengine kufikiri kuna namna wanafanyiwa kuibiwa fedha zao. Labda ameenda sehemu ya biashara, na kujikuta wametumia fedha nyingi kuliko walivyopanga, na hivyo kufikiri labda wamechukuliwa fedha kwa njia za ushirikina, ambayo wanaita chuma ulete.
SOMA; Kubana Matumizi Siyo Mbinu Ya Kutajirika, Mbinu Hasa Ni Hii.
Kitu kimoja ambacho nakuambia ni kwamba, kila kitu kinachokusumbua kuhusu fedha sasa hivi, kinasababishwa na tabia ulizojijengea kwenye fedha. Na ili kuondoka hapo ulipo sasa kifedha, unahitaji kujenga tabia imara zaidi kwenye fedha.
Leo tunakwenda kuangalia tabia moja ambayo itakuwezesha kudhibiti matumizi ya fedha zako. Kwa tabia hii, utaweza kufanya matumizi muhimu na kuweza kuweka akiba ya fedha zako ili kufanya makubwa zaidi.
Lakini kabla ya kuangalia tabia hii, hebu kwanza tuangalie tabia moja inayotusumbua kwenye fedha. Tabia hii ni kufanya maamuzi yanayoendeshwa na mihemko kwenye fedha. Maamuzi haya ya mihemko ni pale unapokuwa na fedha, ukaona kitu, kikakupendeza na kujishawishi kwamba unakihitaji halafu ukanunua. Au unapita mahali, ukiwa na fedha zako, mtu anakuambia kuna kitu anauza, unakiona ni kizuri, na bei anayouza ni rahisi, huwezi kupata popote, na yeye anakusisitiza ukikosa sasa hutapata tena, ghafla unajishawishi kununua, unanunua lakini baadaye unagundua haikuwa muhimu kiasi hicho kwako.
Tabia hii imefanya watu kununua vitu vingi wasivyovihitaji, na wauzaji wengi wanajua kuitumia vizuri. Unapokwenda mahali kununua vitu, hasa kwenye maduka makubwa, ambayo unachagua vitu unavyotaka mwenyewe, unakutana na matangazo mengi yanayosema kitu kipo kwenye promosheni au bei ya punguzo. Haraka unakimbilia kununua, ukiamini hutakuja kupata tena bei kama hiyo. Hivyo ndivyo unavyokuwa umechagua kutumia fedha zako kwa mihemko badala ya kufikiri kwa kina.
Tatizo linakuwa kubwa zaidi kwa sababu wakati mwingine unazidiwa ujanja na wafanyabiashara. Kwa sababu wao wanachotaka ni kuuza, hawataki kujua kama unachonunua unakihitaji kweli au la, wala hawataki kujua kama kitakusaidia au la. Hivyo wao wanachofanya ni kutumia kila mbinu mpaka wahakikishe wamekuuzia kile wanachouza. Wakati mwingine watakufanya uone unakosa kitu kizuri, wakati mwingine watakufanya uwaonee huruma, zote hizo ni mbinu za kisaikolojia wanatumia ili kuangusha upinzani wako wa kununua.
Hivyo unaona kwa namna gani vita hii siyo rahisi kwako, unaweza kujiambia hununui lakini mwisho wa siku ukarudi ukiwa umeshanunua.
Habari njema ni kwamba, ipo njia ya kuondokana na yote haya, ipo njia ya kujikinga na hila zote hizo na kuwa na matumizi mazuri ya fedha zako. Na njia hiyo ni kujifunza tabia moja muhimu sana inapokuja kwenye matumizi ya fedha zako.
Tabia hiyo ni kuwa na subira kwenye kununua kitu chochote ambacho hukuwa umepanga kununua. Yaani unapokutana na kitu ambacho unajishawishi kwamba ni muhimu kununua, usikinunue hapo hapo, badala yake andika mahali kwamba utakinunua. Kisha ondoka, na baadaye utakapopata muda, andika orodha ya faida na hasara ya kununua kitu hicho. Fikiri kwa kina kwa nini unadhani unakihitaji sana kitu hicho. Na kama sababu za kukihitaji zitakuwa kubwa kuliko za kutokukihitaji hapo unaweza kukinunua.
SOMA; Makadirio Ya Matumizi Na Faida.
Ili kuhakikisha unakwenda vizuri na hili, unapotoka kwenda kufanya manunuzi, orodhesha kabisa ni vitu gani utanunua kwenye manunuzi unayokwenda kufanya wakati huo. Na unaponunua tembea na orodha yako, ukishanunua weka alama ya vema. Kwa namna yoyote ile, hata ushawishiwe kiasi gani, usinunue kitu ambacho hakipo kwenye orodha yako. Vile ulivyonavyo kwenye orodha ndivyo vitu unavyohitaji kweli, na ndiyo maana ulitoka na kwenda kununua. Vile utakavyokutana navyo na kushawishika kununua huvihitaji kiasi hicho, umevitamani tu. Hivyo kama kuna vitu utashawishika kununua, orodhesha sehemu nyingine na utakwenda kutafakari na siku nyingine utakapofanya manunuzi ndiyo utatekeleza hilo.
Zoezi hili linaweza kuwa gumu pale utakapokutana na kibao kinasema punguzo asilimia 50, zimebaki chache tu, nunua sasa. Nakuambia siyo kweli, usikimbilie kununua, wakati unapohitaji utapata kwa bei nzuri tu, hata kama hakuna punguzo. Ukifuata hayo matangazo, utanunua vitu ambavyo huhitaji kwa kuamini hutaki kupitwa. Hakuna chochote kinachokupita, hivyo tulizana na fanya kile ambacho ni muhimu kwako kwa wakati husika.
Swali ni je usubiri kwa muda gani kabla ya kununua kitu ambacho umetamani kununua wakati unapita mahali? Hapa jibu inategemea, kitu chenyewe na ukubwa wa gharama zake. Lakini isiwe chini ya masaa 24, hivyo inaweza kuchukua siku mbili mpaka siku 30. Kadiri gharama zinavyokuwa kubwa, jipe muda zaidi. Kwa muda huo pia utafikiria njia mbadala za kupata unachotaka na kwa gharama ndogo zaidi. Ambapo mara zote ukifanya utafiti wako kwa kina, utakutana na ofa ambayo ni zuri zaidi.
Kusudi kuu hapa ni wewe usinunue kitu kwa mhemko, kwa sababu tu umekutana nacho. Bali ununue kitu ambacho unakihitaji kweli, umekifikiria kwa kina na utakitumia. Usiwe mtu wa kununua vitu kwa ushawishi wa wauzaji, ile ndiyo kazi yao, na hawataacha kuifanya. Fedha ni zako hivyo zisimamie vizuri kwenye matumizi yako.
Unaweza kuona zoezi hili ni kujinyima uhuru, kujibana au kujitesa wakati fedha unatafuta mwenyewe. Lakini ukiangalia kwa undani, mateso zaidi yako kwenye kununua vitu ambavyo huvihitaji, kwa sababu tu ya kuridhisha tamaa yako ya muda mfupi.
Fanyia kazi tabia hii kila siku, usiende kununua kitu bila orodha, pia usinunue kitu kwa mara ya kwanza unapokutana nacho, hata kama unajishawishi utakihitaji baadaye. Andika kwenye orodha yako na nenda katafakari. Kama utapata sababu za msingi kabisa za kukinunua, unaweza kufanya manunuzi hayo. Ukianza kufanyia kazi tabia hii, utashangaa namna utakavyopunguza kununua vitu usivyovihitaji.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
