Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu,
Karibu kwenye makala yetu ya leo ya FALSAFA MPYA YA MAISHA, ambapo tunajenga misingi imara ya maisha yetu, ili yawe bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. Kama nikikuuliza falsafa ni nini utanijibu ni nini? Unaweza kujibu uwezavyo, kwa maana za kitaaluma au kihistoria. Lakini naomba ukumbuke kitu kimoja kwenye falsafa, ni kuwa na misingi ambayo unaiishi. Hivi ndivyo wanafalsafa wote wakubwa kuwahi kupita hapa duniani walivyoweza kuacha alama. Walikuwa na misingi, ambayo wala siyo mingi au migumu, na waliishi misingi hii kwenye maisha yao, bila ya kukubali kutetereshwa. Na ukisoma vizuri historia za wanafalsafa hawa, wengi walikubali kuuwawa na kuhukumiwa au kuweka kizuizini kwa sababu ya misingi waliyochagua kuiishi na kuwafundisha wengine.
Leo nina swali moja kwako kama mwanafalsafa, je ipi misingi ambayo umejiwekea kwenye maisha yako, kazi zako, biashara zako na hata mahusiano yako na wengine? Kwa sababu, kitu kimoja ni kwamba, kama huna misingi yoyote ambayo umejiwekea, utajikuta unafanya maamuzi ambayo yatakuharibia maisha yako kabisa, au yatakuletea matokeo ambayo hukuwa unayategemea. Upo usemi kwamba KAMA HAKUNA CHOCHOTE UNACHOSIMAMIA, BASI CHOCHOTE KINAWEZA KUKUANGUSHA. Hii ina maana kwamba, kama hakuna misingi uliyojiwekea, kwamba lazima nifanye hivi au kamwe siwezi kufanya hivi, kuna siku utashawishika kufanya jambo la hovyo na litakuharibia. Kwa kukosa misingi imara unayoifuata, utaangushwa na chochote kile kitakachopita mbele yako na kuwa na ushawishi kwako.
Na nikuambie tu wazi, hakuna kitu kimoja ambacho nimeona kinaangusha watu wengi kama hichi. Unakuta mtu anaanza safari yake ya kikazi vizuri, akijituma kuweka juhudi kubwa ili kujenga jina lake na sifa yake. Lakini kwa kukosa misingi, anashawishika kufanya jambo ambalo linaishia kuharibu kabisa jina lake. Kwenye biashara kadhalika, watu wamekuwa wanakazana kujenga biashara zao, wanajinyima kweli na kufanya kazi zaidi ya kawaida. Lakini wanakuja kufanya maamuzi ambayo yanaharibu kabisa kile ambacho wametumia muda mwingi kukijenga.
SOMA; Maana Halisi Ya Kuwa Mtu.
Kwenye kila eneo la maisha yetu, tunahitaji kuwa na misingi, tunahitaji kuwa na mambo ambayo lazima tuyafanye na mambo ambayo hata iweje, hatuwezi kuyafanya. Lazima sisi kama wanafalsafa tujiwekee miiko yetu binafsi, ambayo tupo tayari kuisimamia na kuitetea bila ya aibu. Kwa kukosa miiko hii, kutatufanya kuangushwa na vitu vidogo na kuharibu kila ambacho tumeshajenga kwenye maisha yetu.
Unahitaji miiko kwenye maisha yako binafsi, hapa unakuwa na mambo ambayo lazima ufanye na ambayo huwezi kufanya hata iweje. Namna unavyoendesha maisha yako lazima iwe inayokuwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio. Namna ambayo itakuwezesha kujenga mahusiano bora na wengine, na kufanya kazi kwa juhudi kubwa.
Kwenye kazi au biashara unayofanya pia, weka miiko yako, jiwekee mambo ambayo lazima uyafanye na yale ambayo ni mwiko kwako kufanya. Hata kama kila mtu atakuwa kinyume kabisa kwa wakati fulani, endelea kusimamia kile ambacho unajua kinakuwezesha wewe kufika kule ambapo unataka kufika. Miiko yako ndiyo itakuwezesha wewe kudumu kwenye jambo lolote unalofanya, bila ya miiko hutafika mbali, kila kona kuna mambo yanajipanga kukuangusha wewe.
Habari zote mbaya tunazosikia kuhusu watu ambao tulikuwa tunawachukulia kwa namna fulani kwenye jamii, lakini baadaye ikagundulika kuna mambo ya ajabu wamefanya, huwa ni kwa sababu walikosa miiko, au walikuwa nayo lakini hawakuwa na nidhamu ya kuweza kuisimamia bila ya kuyumbishwa na kitu chochote kile. Kwa sababu changamoto namna moja ya kuwa na miiko ni kwamba utajaribiwa kuivunja. Majaribu yataanzia ndani yako mwenyewe, kwa hisia na tamaa zako binafsi, zitakutaka uvuke miiko yako ili kupata kile ambacho unatamani kupata kwa wakati huo. Ukishinda haya ya ndani, yanakuja ya nje, na haya ndiyo mabaya zaidi kwa sababu yanaweza kuja na hatari kubwa kwako na ukajishawishi huna namna bali kuvunja miiko yako. Wapo ambao wanavunja miiko hiyo na kuamini wameepuka hatari iliyokuwa mbele yao, mpaka wanapokuja kujikuta wametengeneza hatari kubwa zaidi.
Wale ambao wanapenda kusema wamepitiwa na shetani akawafanya watende yale ambayo hawakutegemea kutenda, ni kukosa nidhamu au kukosa miiko thabiti ambayo inatoka ndani yao binafsi. Kwa sababu changamoto nyingine ya miiko ni kwamba ile inayotoka nje yetu, ni rahisi kuivunja kuliko tunayojitengenezea sisi wenyewe. Miiko ikiwa ni sheria ambazo zimewekwa wengi wanazivunja, lakini miiko inapotoka ndani ya mtu mwinyewe, anachohitaji ni nidhamu tu ya kuweza kuishi miiko yake.
Nirudi kwako mwanafalsafa mwenzangu, ni miiko ipi ambayo umejiwekea kwenye maisha yako? Ni mambo gani ambayo unayasimamia kwenye kila ambacho unafanya? Yapi ambayo upo tayari kuyasimamia kwa gharama yoyote ile? Jihoji maswali haya, na jipe majibu, ambayo utayaandika na kuwa msingi wa maisha yako.
Kama unapojiuliza hupati majibu, basi upo eneo hatari na unahitaji kutengeneza miiko ya maisha yako haraka sana. Usipofanya hivyo, chochote unachokazana kufanya sasa, unapoteza muda wako kwa sababu ni swala la muda tu, kabla hujakutana na jambo litakaloharibu kila unachofanya, kutokana na kukosa miiko unayoisimamia.
Ipo miiko ambayo huenda umefundishwa kwenye jamii uliyokulia au kwenye familia yako. Ipo miiko ambayo huenda umefundishwa kwenye dini yako. Kama hii inakuwezesha kuwa na maisha bora, vizuri sana na igeuze kuwa yako, yaani imiliki. Kuimiliki maana yake unaiishi, kwa sababu umechagua na siyo kwa sababu inakupasa. Unapofanya kitu kwa sababu umechagua unakuwa huru, ila unapofanya kwa sababu imekupasa, unakuwa mtumwa na maisha hayawezi kuwa bora.
Kwa mfano, mara kwa mara kumekuwa na habari za viongozi wa dini kukumbwa na kashfa za uzinzi au ubakaji. Kitu kimoja tunachojua ni kwamba, dini zote zinakataza uzinzi na ubakaji, sasa inakuwaje kiongozi kabisa wa dini afanye hivyo. Na hapo ndipo unapoona nguvu ya kufanya kwa kuchagua na kufanya kwa sababu ni wajibu. Kiongozi yeyote wa dini anayechagua kutokuwa mzinzi kama msingi wa maisha yake, hawezi kujihusisha na uzinzi. Ila kiongozi wa dini ambaye atasema siyo mzinzi kwa sababu utaratibu wa dini hauruhusu, ana nafasi ya kufanya uzinzi, iwapo atajidhihirishia hakuna atakayeweza kugundua amefanya hivyo. Na hivyo hufanya hayo wakifikiri ni siri, lakini kwa kuwa dunia haina siri, inafika wakati yote wanayofanya yanakuwa hadharani.
Hii ndiyo sababu kwa nini miiko ya maisha yako, uimiliki, ufanye au uache kufanya, kwa sababu umechagua na kwa sababu ina maana kwenye maisha yako binafsi. Isiwe ni wajibu, isiwe unafanya ili uonekane na wengine. Unafanya hata kama hakuna anayekuona, na namna hii ndivyo unavyoweza kutengeneza sifa imara kwenye maisha na kuwa na mafanikio yanayodumu.
Ipitie miiko yako leo na kujikumbusha kila mara. Na kama mpaka sasa huna miiko, kaa chini na itengeneze. Usione kujiwekea miiko ni kujinyima uhuru, badala yake ni kujipa maisha yenye uhuru wa kuishi na kufanya vile ambavyo utakuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa na yanayodumu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.
Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.
