Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Nina imani umeshinda mengi leo, na kujifunza mengi pia.
Kwa yale uliyoshindwa, hujashindwa bado kama umejifunza kitu, na hivyo kesho nenda kaweke juhudi zaidi.

Karibu kwenye #GHAHAWA yetu jioni ya leo ambapo tunapeana chakula cha fikra ili kuweza kuweka sawa namna tunavyofikiri.
Kwa sababu kuna makosa mengi ambayo tumekuwa tunafanya kwenye kufikiri na kutupelekea kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi.
Lipo kosa la kufikiri ambapo huwa tuna tabia ya kuona kile ambacho tunapenda kuona sisi.
Tunapopata taarifa fulani, au kujua kitu fulani, basi huwa tunatumia uelewa wetu ule kwenye maamuzi yetu yote yanayofuata.
Umewahi kusikia usemi kwamba ukiwa na nyundo kila unachoona ni msumari? Basi hii ndiyo tunazungumzia hapa, ukishakuwa na uelewa fulani, basi kila kitu unachoona kinaendana na ule uelewa. Hata kama havina uhusiano wa karibu.
Kwa mfano kila umewahi kuvaa nguo fulani ukapata matokeo mazuri kwenye kile ulienda kufanya, ukarudia tena nguo hiyo kwa wakati mwingine na ukapata matokeo mazuri, basi utakuwa unaihusisha nguo hiyo na matokeo mazuri. Unaweza hata kuiita nguo ya bahati kwako.
Lakini ukingalia kwa ndani hakuna uhusiano, ila kinachotokea ni kwamba, unapokuwa umevaa nguo ile, chochote kinachotokea unakitafsiri kuwa matokeo mazuri.
Fikiri kwa kina kwenye mambo yote unayokutana nayo na kuyaona, je ndivyo yalivyo au ndivyo unavyotaka kuona? Na ukitaka kuona kweli, basi unahitaji kuweka kile unachotaka kuona pembeni, unahitaji kuhoji na kudadisi kwa kina. Na hii itakuwezesha wewe kuchukua hatua sahihi badala ya kujifariji kwa kitu kisicho halisi.
Nikutakie wakati mwema rafiki.
Kocha Makirita Amani,
http://www.makirita.info