Tunaishi kwenye zama ambazo mambo yanabadilika kwa kasi kubwa. Zamani mtu alikuwa akipata ajira, ndiyo inakuwa ajira ya maisha yake. Lakini sasa hivi mtu akidumu kwenye ajira miaka mitano ni kipindi kirefu kweli. Mabadiliko ni makubwa sana kwenye kazi na hata kwenye biashara. Hakuna mtu yeyote anayeweza kupanga miaka yake mitano ijayo kwa uhakika, kwa sababu vitu vingi vilivyopo leo, miaka mitano iliyopita havikuwepo. Hivyo kitu kimoja ambacho tuna uhakika nacho ni mabadiliko yapo na yataendelea kuwepo.

 

Wakati mwingine mabadiliko yanaanzia ndani yetu wenyewe, tunajikuta tumechoka ile kazi au biashara ambayo tunaifanya. Haituhamasishi au kutusukuma tena na hivyo kuona kama tumefikia mkwamo kwenye maisha yetu. Hapa ndipo tunafikiria nini tunaweza kufanya na maisha yetu zaidi ya pale tulipofika.

Changamoto ni kwamba, watu wengi hatuna maandalizi ya kuweza kwenda na kasi hii ya mabadiliko. Tumezoea kufanya vile ambavyo tumezoea kufanya mpaka tunapokuja kustuka kwamba tumeachwa nyuma. Hapa ndipo mwandishi Jenny Blake alipotushirikisha uzoefu wake kwenye kubadili kazi moja na kwenda nyingine, au hata biashara moja kwenda nyingine. Yeye mwenyewe aliweza kuondoka kwenye kazi nzuri kwenye kampuni kubwa duniani ambayo ni Google na kwenda kufanya kile ambacho kinamvutia zaidi.

SOMA; Do More Great Work (Acha Kuwa Bize Na Anza Kufanya Kazi Yenye Maana)

Karibu tujifunze pamoja mambo haya ya kuzingatia, kwa sababu mbinu hizi zinamhusu kila mtu, iwe umeajiriwa na unataka kutoka kwenda kwenye ajira nyingine au kujiajiri, na hata kama upo kwenye biashara na unataka kubadili biashara hiyo.

Kwenye kitabu hichi, Jenny anatushirikisha hatua tano za kufuata katika kutoka pale tulipo sasa kikazi au kibiashara na kwenda mbele zaidi. Hatua hizo ni KUPANDA, KUTAFUTA, KUJARIBU, KUANZA NA KUONGOZA. Tutajifunza zaidi kuhusu hatua hizi tano kwenye uchambuzi huu wa kitabu.

HATUA YA KWANZA; KUPANDA.

Hatua ya kwanza ya kufanya mabadiliko ni kupanda, hapa unatengeneza msingi wa mabadiliko yako. Katika hatua hii unajenga maadili yako na kutengeneza maono yako ambayo ndiyo yatakuongoza kwenye mabadiliko yako.

1. Ili kujenga msingi imara wa mabadiliko yenye mafanikio, fikiria kwanza kuhusu maadili yako binafsi, vitu gani unathamini sana, vitu gani upo tayari kufanya na vipi hupo tayari kufanya. Hii itakusaidia kuchagua kitu kinachoendana na maadili yako binafsi.

2. Tengeneza maono yako ya mwaka mmoja kutoka pale ulipo sasa, na jione uko wapi mwaka mmoja ujao. Hii ndiyo itakuwa ramani yako ya kufanyia kazi. Na ni mwaka mmoja tu, usiende zaidi ya hapo kwa sababu utajidanganya. Kutengeneza maono ya miaka mitano ijayo kwenye hatua hiyo, huwezi kujua mambo yatakwendaje katika hiyo miaka mitano.

S0MA; WHY WE WORK (Nadharia Ya Nini Kinawasukuma Watu Kufanya Kazi).

3. Ijue kanuni yako ya furaha, hii itakuwezesha wewe kuweza kuweka juhudi hata pale mambo yanapokuwa magumu. Kila mtu ana kanuni yake ya furaha, kwa namna mwili wake ulivyo. Kwa wengi, kula kwa afya, kupata muda wa kupumzika, kufanya mazoezi na kufanya tahajudi inawafanya kuwa na afya inayowaletea furaha.

4. Angalia historia yako ya kazi, umeshafanya kazi ngapi kufika pale ulipo sasa, ni kazi gani zimekuwa zinakupa furaha ukizifanya, zipi ambazo uhitaji wake ni mkubwa. Hapa utapata kitu gani ufanye kwa baadaye.

5. Tengeneza msingi wako wa fedha kabla ya kuchukua hatua ya kuondoka hapo ulipo sasa, na angalau uwe na kipato cha kukuwezesha kuishi angalau miezi sita. Hii ni kwa sababu kuondoka kwenye kazi au biashara ambayo upo sasa huku huna kipato kabisa, kutakufanya ushindwe kufanya vizuri kwenye kile unachoenda kuanza. Kwa sababu changamoto ya fedha itakusumbua sana.

6. Kama huna akiba ya kukutosha, angalia ni kitu gani cha pembeni unaweza kufanya, ambacho kitakuingizia kipato cha kuweza kuendesha maisha wakati unafanyia kazi kile ambacho ni muhimu zaidi kwako. Unaweza kuwa na biashara ya pembeni ambayo inakusaidia upate fedha ya kula. Kwa njia hii hutakuwa na hofu ya fedha na hivyo kuweza kuweka juhudi kubwa.

7. Hakuna hofu kubwa inayowazuia watu kuchukua hatua kama hofu ya kukosa fedha, ndiyo maana watu wamekuwa wakikubali kukaa kwenye kazia ambazo hawazipendi na zina kipato kidogo kwa sababu ya hofu kama wakitoka wataendeshaje maisha. Ili kuondokana na hofu hii kukuzuia kuchukua hatua, hakikisha mara zote unakuwa na zaidi ya chanzo kimoja cha kipato. Kama huna sasa, anza kujenga chanzo hicho.

HATUA YA PILI; KUTAFUTA.

Hapa unatafuta watu, maarifa na fursa zitakazokuwezesha wewe kufikia maono ambayo umeyatengeneza kwenye hatua ya kupanda.

8. Unahitaji watu ambao watakusaidia wewe kufikia ndoto zako, hivyo chagua ni watu wa aina hani unaohitaji na unawezaje kuwapata. Njia nzuri ya kuwapata watu unaowahitaji, na wanaoweza kukusaidia, ni kuanza na watu ambao tayari wapo kwenye mtandao wako. 

Hawa ni ndugu jamaa na marafiki, angalia wapi wanaweza kukusaidia kisha wape maombi ya kile unachotaka kutoka kwao.

9. Njia nyingine unayoweza kuwafikia watu ni kwa kujijenga jina na sifa kwenye jambo fulani. Hapa unachagua kitu ambacho unaweza kukifanya vizuri, na unaweka juhudi kubwa kukifanya kiasi kwamba watu wanakujua na kuja kwako kupata huduma zako. Hapo inakuwa rahisi kupata watu wanaoweza kukusaidia kwa yale unayohitaji wewe.

10. Unahitaji kuwa na mtu wa kukuongoza (mentor). Huyu ni mtu ambaye ameshafanya kile ambacho wewe unataka kufanya, huyu atakupa maarifa muhimu na kukuepusha kurudia makosa ambayo yeye alishayafanya. Unaweza kuwapata watu hawa moja kwa moja kama wanapatikana. Kama hawapatikani, unaweza kuchagua wale ambao unawakubali sana na kusoma vitabu vyao au kufuatilia maisha yao na kujifunza. Lakini usiige kila wanachofanya, jifunze na kazana kuwa bora.

11. Unahitaji kuwa na bodi ya washauri. Hawa ni watu ambao unawachagua ambao kabla ya kufanya jambo lolote, utaomba kwanza ushauri wao. Wanaweza kuwa watu unaoweza kuwauliza moja kwa moja, kama unaweza kuwapata unaoweza kuwaamini na wanaojali. 

Kama huwezi kupata moja kwa moja, chagua watu unaowakubali na wafuatilia kupitia maisha yao na vitabu vyao. Na kabla hujafanya maamuzi jiulize angekuwa fulani angefanyaje? Hii itakusaidia kuepuka makosa yatakayokurudisha nyuma.

12. Unaweza kutumia mtandao kutengeneza jina lako na hiyo ikakuwezesha wewe kuwafikia wale ambao watakusaidia kufikia ndoto zako. Hapa unahitaji kutumia vizuri mitandao ya kijamii na kuwa na tovuti au blog. Unatumia zana hizi kujijengea jina lako kwenye eneo ambalo wewe ni bora, na kupata wafuasi ambao wanafuatilia kile unachofanya.

HATUA YA TATU; KUJARIBU.

Hapa unafanya majaribio madogo madogo kwenye njia ulizochagua kuelekea wenye maono yako.

13. Baada ya kujenga msingi na kutafuta fursa mbalimbali, utakuwa umepata mawazo ya vitu vingi unavyoweza kufanya. Kuchagua kitu kimoja na kuanza kukifanya moja kwa moja unaweza kushindwa kwa kuwa hujajua kwa undani kila ulichofikiria. Hivyo ni muhimu ujaribu kwanza mawazo yako kabla hujachagua moja.

14. Jiandae kukosea na kushindwa. Katika kujaribu, usikatishwe tamaa na kushindwa au kukosea, hata kama wazo lilionekana zuri wakati unafikiria. Hii ndiyo maana unajaribu, na kazi yako wakati huo siyo kuhukumu, bali kujifunza na kuona kipi unaweza kuanza kukifanya kwa hatua kubwa.

15. Anza kidogo kwa kufanya yale ya msingi. Unapofanya majaribio, usiweke rasilimali kubwa kwenye chochote unachojaribu, badala yake fanya yale ambayo ni ya msingi kabisa kisha angalia watu wanapokeaje kile ambacho umefanya. Kitu ambacho kinapokelewa vizuri kinaonekana tangu unapoanza kufanya, kadiri watu wanavyojihusisha nacho na kukihitaji.

SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.

16. Baada ya kujaribu mawazo mengi ambayo umefikiria kufikia ndoto yako, unahitaji kufanya tathmini. Kwenye tathmini yako tumia vigezo hivi vitatu;

Kigezo cha kwanza; je umefurahia kufanya kitu hicho? Unahitaji kufanya kile ambacho unapenda kufanya, ili uweze kuwa bora.

Kigezo cha pili; je ni kitu ambacho una utaalamu wa kukifanya? Au unaweza kujifunza na kuwa bora zaidi? Ili kufanikiwa, lazima uwe vizuri kwenye kile unachofanya.

Kigezo cha tatu; je ipo nafasi ya kukua zaidi kupitia kitu hicho? Soko lipo kubwa? Unaweza kutengeneza kipato cha kukutosheleza?

Katika mawazo yote uliyojaribu, lile ambalo litakidhi vigezo hivyo vitatu, ndiyo unaweza kwenda nalo hatua ya nne.

HATUA YA NNE; KUANZA.

Baada ya majaribio, utakuwa umeona kipi kinakufaa zaidi na kipi unaweza kutumia kufikia maono yako. Unaanza rasmi kwa kufanyia kazi kile ulichochagua.

17. Ni wakati gani sahihi kwako kuanza? Hili ni swali muhimu kwa sababu watu wengi wamekuwa wanaanza mapema sana na kushindwa, au wanachelewa kuanza na kupitwa na fursa. Ili kujua wakati sahihi kwako kuanza, angalia hatua zile zilizopita. Angalia katika majaribio uliyofanya, wazo lipi unaanza nalo. Pia katika hatua ya msingi, angalia una fedha kiasi gani za kukuwezesha kuacha unachofanya sasa na kuanza kufanyia kazi ndoto yako.

18. Kuanza kuna hofu, hata kama una uzoefu kiasi gani. Hii ni kwa sababu unapoanza kitu chochote kipya, unafanya mabadiliko, na mabadiliko ni vitu vipya ambavyo hatuna uhakika navyo. Hivyo ili kuanza unahitaji ujasiri, na kosa ambalo wengi wamekuwa wanafanya ni kusubiri mpaka wapate ujasiri ndiyo waanze, kitu ambacho huwa hakitokei. Usisubiri ujasiri ndiyo uanze, bali anza na ujasiri utakuja. Mara zote ujasiri unatokana na kufanya.

19. Usijaribu kumfurahisha kila mtu, kufanya hivyo hutaweza kupiga hatua yoyote kwenye maisha yako. Maamuzi yoyote ya kuanza utakayofanya, watawavuruga wengine, kuna ambao watakubaliana na wewe na wapo ambao hawatakubaliana na wewe. Ukitaka kutokuwaudhi wengine, utaendelea kubaki hapo ulipo miaka yako yote. Kama ambao wamebaki kwenye ajira wasizozipenda na hata haziwalipi kwa sababu tu hawawezi kuacha kwa kuwa wazazi au wenza wao watachukia.

20. Kuanza siyo kwamba ndiyo uhakika wa kufanikiwa, unaweza kushindwa pia licha ya kufanya yote ambayo ulipanga vizuri. Hivyo unapokwenda kuanza jiandae, uwe na njia ya kuweza kuendelea hata pale unapokutana na changamoto. Na eneo la kwanza ni kuhakikisha kipato cha kuendesha maisha kipo.

HATUA YA TANO; KUONGOZA.

Hapa unawawezesha wale waliopo chini yako nao kuweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye kazi zao ili nao kuweza kufanya kazi bora zaidi.

21. Kitu kinachowafanya watu wengi kuondoka kwenye kazi zao, ni pale ambao wanaona kazi hizo haziwafai tena, labda wao wanakua kuliko kazi zao, au kazi zao zinakuwa kuliko wao. Hivyo wewe kama kiongozi, unahitaji kuwasaidia wale waliopo chini yako wasifikie hatua hiyo. Na njia ya kufanya hivyo ni kuwasaidia kukua na kazi zao, au kuwawezesha kuboresha zaidi kazi zao. Kama utakuwa karibu na wafanyakazi wako, kwa kujua changamoto zao kwenye kazi, utaweza kuwasaidia na wakawa bora zaidi badala ua kuondoka.

Hizi ndizo hatua tano muhimu za kufuata kama unataka kufanya mabadiliko kwenye kazi au biashara yako. Kutoka hapo ulipo sasa na kupiga hatua zaidi kunahitaji mikakati mizuri na uvumilivu pia. Na muhimu zaidi, hutafanya mabadiliko hayo tu kwenye maisha yako, jiandae kwa mabadiliko mengi kwa sababu dunia inazidi kubadilika kila siku.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita