Habari za siku yako ya leo rafiki?
Je yapi makubwa uliyofanya leo?
Na zipi changamoto zimekufanya ujifunze zaidi?
Usisahau kupitia haya kabla hujamaliza siku hii nzuri.

Karibu kwenye #GHAHAWA ☕ ☕ jioni ya leo,
Kupitia ghahawa tunachangamsha akili zetu ili kuweza kufikiri sawasawa na kuacha kufanya makosa yanayotugharimu.

Leo nianze na swali,
Umewahi kwenye kwenye duka la vitu na ukakuta kitu kimewekewa bango PUNGUZO LA ASILIMIA 50, LEO TU!! Na ukajikuta unakinunua hata kama hukuwa na mpango wa kukinunua? Labda ni kitu ambacho unakihitaji kweli, lakini hukuwa umepanga kukinunua siku hiyo, ila kuwa kina punguzo, ukanunua.
Sasa swali zuri zaidi ni hili; je ulikuwa unajua bei ya kitu hicho kabla hujaambiwa kina punguzo?
Wapo wafanyabiashara wamekuwa wanaweka tangazo la punguzo kwa asilimia kumbe hakuna punguzo lolote. Lakini watu wananunua kwa wingi, kwa sababu wanalinganisha bei halisi na bei ya punguzo, wanaona bora wachukue hatua haraka.

Tumekuwa tunafanya kosa hili kwenye maeneo mengi sana ya maisha yetu, kufanya maamuzi kwa msingi wa kulinganisha, na siyo msingi wa uhitahi au ubora.
Na watu wanaonufaika na hili ni wafanyabiashara.
Kwa mfano, ukienda kununua begi la kubebea kompyuta pekee, na ukaambia bei yake ni elfu 50, utaona ni nyingi, na kuamua labda uangalie aina nyingine au mahali pengine. Lakin ukaenda kununua kompyuta, labda ya milioni moja, na ukaambiwa kuna begi la elfu 50, hutaona ni ghali. Hii ni kwa sababu unalinganisha milioni moja uliyotoa na elfu 50 unayoambiwa utoe, huoni ni kubwa. Lakini elfu 50 ni ile ile, haijabadilika, kilichobadilika ni wewe unailinganisha na nini 😀😀

Fikiria makosa mangapi umekuwa unayafanya kwa kulinganisha hivyo.
Kuondokana na hili, hakikisha kila uamuzi unaofanya, unajitegemea wenyewe. Kamwe usifanye maamuzi kwa sababu ya kitu kingine ambacho kinakusukuma wewe kufanya maamuzi hayo.

Nikutakie wakati mwema.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
http://www.makirita.info