Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu,

Karibu kwenye makala yetu nyingine ya falsafa mpya ya maisha ambapo tunajenga falsafa mpya ya maisha yetu ili kuweza kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Kwenye jamii zetu, huwa kuna pande mbili ambazo mara zote zinakinzana, na tunaweza kusema ni sheria ya asili, kwamba kila kitu kina upacha. Kama ilivyo usiku na mchana, baridi na moto, wake na waume. Hivyo mambo mengi yamekuwa yanaangukia kwenye pande kuu mbili.

Kwenye kila jambo, upo upande unaokubaliana nao na upo upande ambao unapingana na jambo hilo. Ni kila jambo, haijalishi kama ni zuri au baya. Bali watu watapingana, ni sheria ya asili kabisa. Na mara nyingi hakuna upande unaokuwa sahihi zaidi ya upande mwingine. Yaani kila upande unakuwa sahihi, kutokana na namba wanavyoona kitu husika na mtazamo walionao. Ndiyo maana hata kama watu watabishana vipi, bado kila mtu ataendelea kuwa upande aliopo.

Tuchukulie mfano wa dini, kwenye jamii zetu dini kubwa ni Uislamu na Ukristo, kunaweza kuwa na makundi mengine, lakini hayo utaona ndiyo makubwa. Sasa Wakristo wataona wao ni sahihi zaidi na Waisilamu wanakosea. Kadhalika Waislamu nao watakuwa wanawaona Wakristo kwamba wanakosea na wao ndiyo wapo sahihi. Ni mpaka utakapoingia kwenye falsafa za pande hizo mbili, ndiyo utaelewa kwa nini kila upande unaona upo sahihi na upande mwingine unakosea. Hivyo kwa uhalisia, kila mtu yupo sahihi, kulingana na falsafa ambayo amechagua kuishi.

Tukija kwenye maisha ya mafanikio, kuna pande mbili za falsafa.

Wapo wale ambao wanaamini kwenye kuweka juhudi kubwa ili kuwa na mafanikio makubwa ya maisha yao. Kuwa na mipango ya siku zijazo na kujiandaa kwa siku hizo, kabla hata hazijafika. Watu hawa wanajua kwamba hakuna kinachopatikana kirahisi, unahitaji kuumia kwa kiasi fulani ili kuweza kupata yale makubwa ambayo mtu unataka kwenye maisha yako. Wanajua pia kwamba kuna kushindwa na wanaposhindwa wanainuka na kuendelea tena na tena mpaka wapate kile wanachotaka. Huu ni upande wa kupambana, na hautafuti lawama bali kupambana kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Upande wa pili ni wa wale watu ambao wanaishi leo, na kesho itajijua yenyewe. Hawa ni wale watu wanaoangalia wanavukaje leo tu, kesho kama watakuwepo basi wataihangaikia kama ilivyo leo. Hawana mipango mikubwa ya mbele na wala hawapo tayari kuweka juhudi kubwa ili kuboresha zaidi maisha yao ya mbeleni. Hawaamini kwenye kuweka juhudi kubwa, hivyo wanachoangalia wao ni njia ipi rahisi ya kupata kile wanachotaka bila ya kuweka juhudi kubwa. Hawapo tayari kuumia na hivyo hawafanyi chochote cha kuwaumiza ambacho pia kingeweza kuwanufaisha zaidi. Pale wanapojaribu kitu wakashindwa, huacha mara moja na wala hawajaribu tena. Na kwa kila changamoto wanayopitia, wanajua kila mtu wa kulaumiwa kwa kuwafanya wafike hapo.

SOMA; Ukweli Siyo Kipaumbele Cha Wengi, Na Kwa Nini Ni Muhimu Zaidi Kwako.

Hizi ni pande mbili za falsafa na ukiangalia jamii, watu wanaangukia upande mmoja au mwingine. Lakini kwa sehemu kubwa, watu wapo kwenye falsafa ya maisha yasiyo ya juhudi wala mateso. Upande wa kulaumu serikali, ndugu, wazazi na hata mvua kwenye kushindwa kupata kile wanachotaka. Upande wa juhudi hauna watu wengi, wengi hawauwezi kwa sababu haubembelezi, una mateso ambayo yanamtaka mtu awe amejitoa kweli.

Sasa changamoto ambayo nimeona inawasumbua wengi ni hii. Mtu anakuwa kwenye upande mmoja wa falsafa, ule upande ambao hauhitaji juhudi. Maisha yanakuwa magumu zaidi kwake, anaona hayafai, anatafuta namna ya kutoka pale alipo. Anakutana na falsafa ya juhudi, anaona inamfaa, anaanza kuifanyia kazi, anakutana na changamoto, anarudi kule alipotoka. Au anapoamua kuyabadili maisha yake, na kuanza kuweka juhudi kubwa, wale wanaomzunguka wanaanza kumkatisha tamaa, na kumuuliza anahangaika nini kiasi hicho, na yeye anajiangalia na kuona bora arudi kule alipozoea.

Hapa ndipo nataka nikukumbushe kwamba, usichanganye falsafa, kama ambavyo huwezi kwenda msikitini ijumaa, halafu jumapili ukaenda kanisani, hivyo pia kwenye falsafa zako zote za maisha, chagua upande mmoja, na nenda nao huo, utekeleze kwa uhakika na utavuna kile unachotafuta. Usichanganye falsafa, usijaribu huku wakati unaamini upande mwingine, utajivuruga na kushindwa kupiga hatua yoyote kubwa kwenye maisha yako.

Kitu kimoja nimegundua ni kwamba, wale wanaochanganya falsafa, ndiyo ambao siku zote wamekuwa wanadanganywa, wanatapeliwa na hata kuibiwa. Naona hili kwa watu wengi, hata wanaojifunza kupitia kazi zangu.

Falsafa yangu kwenye fedha ni hii; kwamba fedha inapatikana baada ya kuwa umetoa thamani kwa wengine. Na ili kutoa thamani, lazima ufanye kazi, ambayo itazalisha bidhaa au huduma ambayo inawasaidia wengine. Kwamba hakuna njia ya mkato na ya haraka ya kupata fedha kama hakuna kazi inayofanyika. Sasa anakuja mtu kukuomba ushauri, kuna hii biashara nimeambiwa unapata faida ya haraka bila hata ya kufanya kazi. Namuuliza ni thamani gani ambayo wewe unatengeneza kupitia biashara hiyo inayokufanya ustahili kulipwa fedha hizo? Ananiambia, sijui, lakini naona watu wanapata fedha. Hapa ndipo unagundua wengi hawajachagua falsafa, bali wanajaribu kutafuta mteremko uko wapi. Kwa bahati mbaya mteremko haupo na wanaishia kutapeliwa au kupoteza muda, fedha na hata uaminifu wao, baada ya kujihusisha na mambo ambayo siyo halali.

Uzuri wa kuchagua falsafa na kuisimamia ni kwamba, hakuna atakayeweza kukuyumbisha. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu na kunitapeli kwa namna yoyote ile, hata kama ni tapeli aliyebobea dunia nzima. Siyo kwa sababu nina akili kushinda watu wengine wote, ila kwa sababu nimechagua falsafa ambayo naiishi kila siku. Hivyo kitu kikija narudi kwenye misingi, je kinaendana na misingi ninayosimamia? Kama hakiendani basi naachana nacho, siangalii kama nchi au dunia nzima inakubaliana nacho, ninachoangalia ni misingi ninayoiamini mimi ndiyo sahihi. Ukiangalia wengi wanaonufaika, wau wengi wanaokubaliana na kitu, utayumbishwa kila wakati.

Hivyo mwanafalsafa mwenzangu, chagua falsafa utakayoiishi na usichanganye falsafa. Ijue vizuri falsafa unayoiishi, ijue misingi ya falsafa hiyo na usisumbuke tena na mambo madogo madogo. Kama kitu kinakwenda kinyume na misingi unaachana nacho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog