Hakuna ambaye hapendi kufanya mambo makubwa kwenye maisha yake. Na kuonesha ni namna gani tumejitoa kufanya makubwa, tunapanga kabisa kila tunachotaka kufanya na kuona wapi tunapotaka kufika. Lakini hii ni sehemu rahisi ya kufika tunakotaka, tunaweza kusema ni asilimia moja pekee. Sehemu kubwa, ile asilimia 99, inatokana na juhudi tunazoweka ili kupata kile tunachotaka, kufika pale tunapotaka kufika, na hapo ndipo penye changamoto kubwa, ndipo wengi wanaposhindwa na kuachana na safari waliyoianzisha.
Inakuwa vigumu na changamoto kuwa kubwa kwa sababu ya mambo mengi, lakini machache makubwa ni haya;
- Asili yetu wenyewe kama binadamu.
Kwa asili sisi binadamu ni wavivu, tunapenda kupata tunachotaka, lakini hatupo tayari kuweka juhudi kubwa au kuumia kwenye kupata kitu hicho. Hivyo mara zote tumekuwa tunatafuta njia ya mkato na ya haraka ya kupata tunachotaka, bila ya kuweka kazi kubwa na kuumia. Ndiyo maana ukiangalia watu wengi, wanafanya vitu vinafanana, kazi biashara na kila kitu. Kwa sababu ni rahisi kuiga kile wengine wanafanya, kuliko kuanzisha kitu kipya.
Asili yetu hii imekuwa kikwazo kikubwa kwetu, kwa sababu hakuna jambo kubwa linalopatikana bila ya kuweka juhudi. Haipo njia ya uhakika ya kufanikiwa kwa haraka bila ya kuweka kazi na kuumia. Watu wamekuwa wakipoteza muda kwenye njia zisizo sahihi na hili linaharibu kabisa mafanikio yao.
- Watu wanaotuzunguka.
Hakuna watu hawapendi kukuona wewe ukifanikiwa kama wale wanaokuzunguka. Unaweza kubisha hilo lakini inabidi uelewe ni mafanikio gani naongelea hapa. Ni yale mafanikio ya kufanya jambo kubwa la ndoto za maisha yako, kujaribu mambo makubwa ambayo wengine hawajawahi kufanya kabisa. Sasa utakapowaambia watu au utakapojaribu kufanya, watakuja na kila sababu ya kukuzuia, kwamba haiwezekani, kwamba hujajiandaa vya kutosha, kwamba utashindwa, na hadithi nyingine zitakazokukatisha tamaa.
Kwa uhalisia watu hawa unaweza kuwaona kama wanakupenda hivi, na hata wao wenyewe watajua wanafanya hivyo kwa sababu wanakupenda. Ila ukweli ni kwamba wanafanya hivyo kwa sababu hawataki ufanye makubwa. Kwa sababu ukifanya makubwa, wao wataonekana ni wazembe, kwa nini na wao hawawezi kufanya kama ulivyofanya wewe? Jaribu kupata picha umeajiriwa mahali, umekuta kuna watu wapo pale miaka mingi, ukaona kipo kitu kinaweza kuboreshwa zaidi, unafikiri ukitoa wazo hilo watalichukuliaje? Lazima walipinge sana, wataonesha namna gani wazo hilo ni hatari, na litaonekana haliwezekani. Sasa hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila eneo la maisha. Unapojaribu kufanya vitu watu hawajawahi kufanya, hawajisikii vizuri sana, na hivyo kukuzuia usifanye.
Wakati mwingine watu hasa wale wa karibu, wanakuzuia usifanye kwa sababu wanaogopa ukishindwa utakuwa mzigo kwao. Hivyo wanakutaka ucheze salama na mambo yako yaendelee kuwa kawaida, kuliko kujaribu kitu cha hatari, kinachoweza kukupa makubwa, lakini pia kikawa na hatari ya kukuangusha.
SOMA; Haraka Ya Zama Hizi Itakupoteza…
- Usumbufu na kelele za kila aina.
Nikuulize swali moja, ni mara ngapi unaishika simu yako kwa siku? Labda hilo linaweza kuwa gumu, kwa kushindwa kuhesabu mara zote. Labda tubadili swali, inakuchukua muda kiasi gani kabla hujashika simu yako? Hapo ni iwe umepigiwa au la. Tafiti nyingi zinaonesha, watu hawawezi kukaa dakika 10 bila ya kushika simu zao. Na hii yote ni kutokana na mitandao ya kijamii na mtandao wa intaneti, mikono yetu ni kama imefungiwa kwenye simu zetu. Hata kama simu haijaita, utaichukua na kuchungulia kwenye mtandao kuna lipi jipya. Hata kama umetoka kwenye mtandao huo dakika 5 zilizopita!
Simu zetu na mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikuu cha usumbufu na kelele kwetu binafsi. Imekuwa ni vigumu sana mtu kuweza kuweka mawazo yake yote kwenye kazi anayofanya, kwa muda mrefu, angalau saa moja na kuendelea. Kutokana na kugawanyika kwa mawazo yetu, nusu kwenye kazi, nusu tunawaza simu, ufanisi wetu unapungua. Kutokana na usumbufu wa kukatisha kile tunachofanya ili kuangalia simu zetu, tunashindwa kukamilisha mambo makubwa tunayotaka kufanya.
Usumbufu huu umekuja na gharama kubwa, kikazi, mahusiano na hata muda. Watu sasa hawawezi kukaa pamoja muda mrefu wakaongea, mtu kwa mtu. Dakika chache na kila mtu yupo kwenye simu yake.
Haya ndiyo matatu makuu yanayotuzuia kufanya mambo makubwa kwenye maisha yetu, yatakayotupelekea kufanikiwa.
Sasa dawa yake ni nini?
Dawa kuu ni moja; NG’ANG’ANA NA KATAA.
NG’ANG’ANA.
Chochote ambacho unataka kufanya kwenye maisha yako, lazima uwe king’ang’anizi. Lazima utake kweli kiasi cha kuweza kuvuka kila changamoto itakayokuja mbele yako.
Lazima uwe unakitaka kiasi kwamba asubuhi usingizi unakatika kabisa na unahamasika kutoka kitandani ili kwenda kuweka juhudi ili kupata unachotaka.
Ng’ang’ana kuweka juhudi kubwa kila siku, kufanya kila unachopaswa kufanya ili kuweza kupata kile ambacho unataka kupata. Jua kabisa kwamba itakuchukua muda, utahitaji kuumia kwa namna moja au nyingine ili kupata unachotaka.
KATAA.
Kataa kabisa usumbufu wa aina yoyote ile. Panga muda wako wa kufanya kazi zile muhimu, na muda huo ulinde. Ndani ya muda huo usishike simu, wala usitembelee mitandao yoyote. Weka mawazo yako yote kwenye kazi ile unayoifanya, na hata kama kuna changamoto yoyote, haitaweza kukushinda. Tenga muda ambao hauna usumbufu, labda usiku sana au asubuhi sana, kulingana na unavyoweza wewe. Asubuhi sana ni muda mzuri, ukiamka saa kumi asubuhi na ukatenga saa moja au masaa mawili kufanya kitu ambacho unataka kuwa bora, au hata kujifunza tu, utakuwa bora sana. Huo ni muda ambao hutegemei mtu yeyote akupigie simu na usiingie kwenye mitandao.
Kataa pale watu wanapokukatisha tamaa, usikubaliane nao kabisa, na wala usiwabembeleze. Kataa mawazo yao na wakatae wao kabisa, kama wanaendelea kukusumbua na mawazo yao. Kataa kabisa wazo lolote la kushindwa kuingia kwenye akili yako, na hii itakuwezesha kusonga mbele zaidi.
Kataa kabisa mwili wako unapokuhadaa kwamba huwezi kuendelea tena na hivyo acha au pumzika. Mwili wako haupendi kuumia, hivyo ukiusikiliza sana hutaweza kufanya makubwa, weka juhudi, na usukume mwili wako zaidi. Wachezaji wote bora, iwe wa mpira au hata riadha, wanajua siri hii muhimu, muda sahihi wa kuanza kuhesabu mazoezi yao, ni pale mwili unapoanza kuuma. Hapo ndiyo wanajiambia wameanza mazoezi. Maana huo ndiyo wakati mwili unawashawishi wasiendelee, huku wao wakijua kuendelea kwao ndiyo kunawatofautisha wao na wale ambao ni wa kawaida tu. Nawe pia usiuendekeze mwili wako, jua kipi unahitaji kufanya na kwa muda gani, na kifanye, kaa pale na kifanye kama ulivyopanga kufanya. Mwili ukishagundua hujisumbui na uvivu wake, unaachana na wewe na hivyo utaweza kufanya zaidi. Lakini ukiwa mtu wa kukubali haraka pale mwili unapokuambia umechoka, mwili unazoea na hutaweza kufanya lolote kubwa.
Ng’ang’ana na kataa, itumie kauli mbiu hii kila siku yako ya mafanikio. Jikumbushe ugumu wa njia, lakini zaidi jikumbushe zawadi ya ushindi, ambayo unaiishi kila siku kwa kufanya kile unachopenda kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
