Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio,
Hongera kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Leo ni siku ya kipekee sana kwetu, tunayo nafasi ya kwenda kufanya makubwa na tutegemee kupaga matokeo bora kutokana na juhudi kubwa tulizoweka.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kuianza siku na maneno chanya.
Tunaishi kwenye jamii ambayo imejawa na habari nyingi hasi. Watu wengi wanaotuzunguka wanaona mabaya zaidi ya mazuri. Hili linaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa mafanikio yetu.
Hivyo tunapaswa kuliepuka kwa juhudi kubwa.
Na njia pekee ya kufanya hivyo ni kuianza siku yako ukiwa chanya.
Ianze siku kwa salamu chanya,
Ianze siku kwa maelezo chanya ya kile ambacho unakwenda kufanya.
Na ianze siku ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kuweka juhudi.

Umewahi kuangalia mchezo wa ngumi?
Kabla ya mchezo kila mchezaji hutamba kwamba atampiga vibaya sana mwenzake. Hutasikia mchezaji akisema, nashiriki tu lakini nigapigwa. Kila mmoja hujitamba atamkomesha mwenzake. Lakini mara nyingi, mmoja kati ya hao hupigwa.
Kwa kuanza na mtazamo chanya wa kwenda kushinda, kunampa kila mpiganaji hamasa ya kuingia ulingoni.
Maisha ni ulingo wa milele, bila ya mtazamo chanya ugapokea makonde ya kutosha kila siku. Hivyo, kila siku ingia ulingoni ukiwa na mtazamo chanya, mtazamo wa ushindi.

Unapoianza siku yako, anza kwa mambo chanya.
Epuka habari,
Epuka mitandao ya kijamii.
Ilishe akili yako lishe bora kabisa ya mafanikio, ambayo ni chanya.
Na nenda kaianze siku yako ukiwa chanya na hamasa ya kufanikiwa.

Nakutakia siku bora sana, ukafanye makubwa leo kwa juhudi kubwa ulizoweka.
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambao ndiyo msingi imara wa mafanikio yetu.

Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
#PAMBANA

MUHIMU; KILA ASUBUHI TUNAPOAMKA, TUWEKE SALAMU ZETU CHANYA HAPA KWENYE KISIMA CHA MAARIFA. NI NJIA NZURI YA KUHAKIKISHA KWAMBA TUMEIANZA SIKU YETU VYEMA. ULE MUDA UNAAMKA TUPEANE SALAMU CHANYA HAPA, ITATUSAIDIA SANA KUIANZA SIKU VYEMA