Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku ambayo umeisubiri kwa shauku kubwa, ulijiambia kesho utafanya, sasa kesho yenyewe ndiyo hii, hakuna nyingine tena.
Msingi wetu mkuu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunaweza kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kunusu HARD WORK au WORKING HARD, vyovyote unavyopenda kuita.
Mafanikio yoyote tunayotaka, yako upande wa pili wa kazi.
Fedha zipo upande wa pili wa kazi.
Chochote unachota, kipo upande wa pili na kazi.
Hii ina maana kwamba kile unachotaka sasa, lakini huna kimetenganishwa na na wewe na kazi.
Hivyo njia pekee na salama ya wewe kupata kile unachotaka, ni kuweka kazi.
Hakuna mbadala wa hilo.

Sasa siku hizi dhana ya kufanya kazi kwa bidii kubwa kama watu hawaipendi hivi. Ni kama watu wanatafuta siri iliyojificha, ambayo wanaamini wachache wanayo, siri hiyo ni kupata makubwa bila ya kufanya kazi. Lakini nasikitika kukuambia hakuna siri ya namna hiyo. Siri ni kazi pekee, ambayo ipo wazi kabisa.

Ukuaji wa teknolojia nao umeendelea kuwahadaa watu. Utawasikia watu wakisema DO NOT WORK HARD, WORK SMART. Yote hayo ni maneno ya kujibembeleza tu, unahitaji kuweka kazi, tena siyo kazi ya kawaida, ni kazi hasa.

Kila kitu kwenye maisha yako kinahitaji KAZI…
Kazi yako inahitaji KAZI…
Biashara inahitaji KAZI….
Mahusiano yanahitaji KAZI…
Utu wako unahitaji KAZI…
Ni kazi, kazi, kazi rafiki, hakuna mkato, hakuna mteremko.
Hivyo ukiwa mjanja, ipende kazi, ipende sana. Watu wakija kwako na njia za mkato, kataa, wewe weka kazi.
Watakucheka kwa muda, lakini wewe ndiye utakuwa na kicheko kikuu mbeleni.

Nikuache sasa ukafanya kazi rafiki yangu,
Uwe na siku njema, ufanye kazi kubwa leo.

Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.
http://www.makirita.info