Kitu pekee ambacho unaweza kukipata kwa mpumbavu ni matatizo, hakuna la ziada. Maana mpumbavu hufurahia kuleta matatizo kwake mwenyewe na kwa wengine pia. Hivyo ni muhimu sana uweze kumjua mpumbavu na kumwepuka kabisa, na kama kwa bahati mbaya ukamjua wakati umeshaingia ‘anga zake’, basi uweze kujitoa haraka.

Kwenye maisha yetu tumezungukwa na wapumbavu wengi, na kibaya zaidi kuhusu wapumbavu ni kwamba hawajijui kama ni wapumbavu. Yaani wao wanaona ni maisha yao ya kawaida, kumbe ni maisha ambayo hayafai kwao na kwa wengine pia.

Kutokumjua mpumbavu ni hasara kwako wewe na siyo kwake, kwa sababu kama usemi maarufu wa Kiswahili unavyokwenda, ukipigana na nguruwe, wote mnachafuka, lakini kwa nguruwe itakuwa furaha kwake. Hivyo unapojikuta kwenye mkwaruzano wowote na mpumbavu, ni lazima utaingia naye kwenye mkwaruzano kama bado hujamwelewa, mnaweza kuambiana mambo mabaya, lakini mpumbavu atakuwa anafurahia, huku wewe ukiumia na kuchafuka.

Hivyo rafiki, nina imani una kila sababu ya kumjua mpumbavu, na huenda ikawa na wewe kwenye baadhi ya mambo ni mpumbavu, hivyo pia hapa itakusaidia kuficha upumbavu wako. Ndiyo upo uwezekano kuwa wewe ni mpumbavu kwenye baadhi ya maeneo, na unakuwa upumbavu pale unapokataa kwamba una upumbavu. Ila ukishakubali, maana unabadilika na kuwa mjinga.

Ipo tofauti ya mjinga na mpumbavu, kama ambavyo tutakavyoona hapo chini.

Mpumbavu ni mtu ambaye hajui kitu, ila pia hajui kama hajui. Kwa sababu hiyo, huamini anajua kila kitu na yeye pekee ndiye aliye sahihi. Wapumbavu huwa na kujiamini kulikopitiliza kwa mambo ambayo hawawezi kuyadhibitisha. Na huwa hawataki kupingwa kwa namna yoyote. Njia yao pekee ndiyo sahihi, za wengine zote siyo sahihi na hazifai.

Mjinga ni mtu ambaye hajui, ila pia anajua hajui, hivyo kuwa tayari kujifunza. Mjinga anapokuwa na jambo na akaambiwa siyo, hakazani kulazimisha ndiyo, badala yake hutaka kujifunza zaidi. Mjinga hajiaminishi kwa mambo ambayo hawezi kuyathibitisha. Mjinga huwa na kitu na akioneshwa ushahidi unaopingana na alichonacho yeye, huwa tayari kujifunza.

Kwa msingi kabisa, hiyo ndiyo maana ya mpumbavu na mjinga. Na kama ulivyoona hapo, ni bora kuwa mjinga kuliko kuwa mpumbavu. Maana mpumbavu ni kama hasaidiki yaani, anaweza kuwa anapotea, na asisikie kile anaambiwa.

SOMA; Muogope Sana Mtu Huyu….

Zifuatazo ni njia ambazo unaweza kuzitumia kumtambua mtu mpumbavu.

  1. Kujua kila kitu.

Dalili ya kwanza na kubwa ya mpumbavu ni kujua kila kitu, hata vile ambavyo kwa hakika havijui. Anaamini kila kitu anakijua, na hivyo kuweza kuchangia kwenye kila jambo. Kila jambo linaloongelewa mpumbavu hakosi maoni yake, na huamini maoni yake yeye ni sahihi. Mpumbavu hubishana na wengine kwenye kila jambo, akijaribu kutetea upande wake ambao hata haujui vizuri.

  1. Mtu wa kujitetea.

Mpumbavu hata siku moja huwa hakosei, na jambo lolote linapoharibika kwake, yupo mtu anayehusika. Kwenye kila jambo ana sababu kwa nini yeye hahusiki na wengine ndiyo wanahusika. Mpumbavu huwa hakosi sababu, hata kama haina uhusiano, ataitumia kama sababu. Mara nyingi hutumia sababu ambazo kila mtu anatumia. Kwa mfano; hali ya uchumi ni mbaya, kila mtu anajua. Mpumbavu atatumia sababu kama hiyo kujiaminisha kwa nini hana fedha.

  1. Hawezi kusikiliza.

Hakuna kitu kigumu kwa mpumbavu kama kukaa kimya na kumsikiliza mtu mwingine akiongea bila ya kumkatisha. Wakati mtu ameanza kuongea, kabla hata hajamaliza, ameshadakia na kumsaidia kumalizia kile alikuwa anasema. Au anamkatisha na kuongea yeye zaidi. Kama ni kwenye malumbano au ubishi, wakati mwenzake anaongea, mpumbavu hasikilizi, bali anatafuta anamjibu nini. Kwa njia hii mpumbavu haelewi na hivyo hata kuongea naye ni kupoteza muda.

Mpumbavu ni mgumu sana kubadilika. Akishashikilia jambo, atakwenda nalo hivyo hivyo, hata kama ushahidi unaonesha hayupo sahihi, huamini yeye yupo sahihi. Kwa njia hii hupotea kabisa kwa sababu ya kutokuwa tayari kubadili mawazo na msimamo.

  1. Kukwepa majukumu.

Mpumbavu hapendi kupewa majukumu, hutumia muda na nguvu kubwa kukwepa majukumu yake.

  1. Kutafuta njia ya mkato kwa gharama ya wengine.

Mpumbavu hutafuta njia rahisi ya kupata kile anachotaka, na hata kama njia hiyo inawaumiza wengine yeye hajali, anachojali ni yeye kupata anachotaka, kwa urahisi. Hivyo huiba, hudhulumu, huchukua rushwa na mengine mabaya ili kupata anachotaka.

SOMA; Giza Haliwezi Kupona Hapa…

  1. Majungu na umbeya.

Hapo ndiyo nyumbani kwa mpumbavu. Hupenda kufuatilia maisha ya wengine, huwajua wengine kuliko anavyojijua yeye. Hutumia muda mwingi kusambaza habari za wengine, kuliko anaotumia kwenye mambo yake mwenyewe.

  1. Kutaka wengine wawafuate wao.

Wapumbavu hutaka wengine ndiyo wawafuate wao, au wafanye kile ambacho wao wanapaswa kufanya. Kwa mfano, ukigombana na mpumbavu, hata kama yeye ndiye aliyeanza matatizo, atataka wewe ndiye umwombe msamaha na umnyenyekee. Hupenda wengine ndiyo wawavumilie wao, na wao hawawezi kuwavumilia wengine.

Wapumbavu wana wivu, wakiona umefanya kitu, badala ya wao kupata hamasa ya kufanya, wanachofanya ni kukuchukia wewe uliyefanya. Wanaona kupata kwako ni kama kunawazuia wao kupata. Utashangaa tu anabadilika, labda mlikuwa karibu kabla hujafanikiwa, lakini baada ya kufanikiwa wewe visa vinaanza. Anataka wewe unyenyekee yeye kwa sababu alikujua kabla hujafanikiwa, wakati mwingine anataka wewe ufanye kile ambacho anakuambia ufanye.

  1. Kukuza mambo.

Wapumbavu huchukua jambo dogo na kulikuza kupita kiasi. Mnaweza kupishana kauli kwa jambo la kawaida tu, lakini mpumbavu ataanza kukuambia maneno makali, huenda hata akakataa kabisa kuongea na wewe tena. Unaweza kujiuliza tatizo ni hilo tu au kuna kitu kingine, hapo jua upumbavu upo kazini.

Hizi ni dalili za wazi kabisa zinazoonekana kwa wapumbavu. Na kama nilivyosema awali, huenda baadhi ya tabia hapo umekuwa unakuwa nazo mara moja au mara kwa mara. Jitambue mapema pale unapokuwa mpumbavu na jirekebishe haraka. Kwa kujitambua na kujirekebisha unaepuka kuonekana mpumbavu kwa wengine na pia kuweza kujifunza.

Na kwa upande wa pili, unapokutana na mtu mwenye hizo tabia, kaa naye mbali, hachelewi kukuletea matatizo makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog