Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.


Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NEXT MOVE, au tukio linalofuata.
Iko hivi rafiki, watu wengi wanapopata kitu cha kufanya, iwe ni kazi, biashara au sanaa, huridhika na kitu hicho haraka na kuanza kukifanya kwa mazoea.
Utawakuta wapo pale pale kila mwaka wakifanya kile kile.
Kwa sababu ndiyo kitu ambacho wameshajua kina matokeo mazuri kwao.
Lakini kama tunavyojua, mabadiliko yapo na yanaendelea kuwepo. Mabadiliko yanakuja kwa kasi na hayamuachi mtu yeyote.
Hivyo kufanya kitu kile kile kwa njia ile ile kwa muda mrefu, unakuwa unaachwa nyuma na mabadiliko.

Kuondokana na hali hii, unaoaswa kuwa na mtizamo wa NEXT MOVE,
Popote ulipo, jiulize ni kipi kingine unaweza kufanya, ni hatua gani muhimu unahitaji kupiga. Kwa namna hii utaziona fursa nyingi zaidi ambazo zitakuwezesha kuwa mbele ya mabadiliko.

Popote pale ulipo, unaweza kwenda mbele zaidi, unaweza kuwa bora zaidi, unaweza kutoa thamani zaidi na unaweza kutengeneza kipato zaidi. Ni wewe kuona kipi unaweza kufanya zaidi na kufanya.

Mambo muhimu kutafakari asubuhi hii;
Je hapo ulipo sasa, umekuwa hivyo kwa kipindi kirefu kiasi gani?
Je ni maeneo gani unaweza kupiga hatua zaidi, unaweza kuwa bora zaidi na unaweza kutoa thamani zaidi?

Kila wakati angalia hatua ipi mpya unaweza kupiga, na hii itakuwezesha kuwa mbele ya mabadiliko.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info