Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo rafiki.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUTATUA TATIZO….
Dunia ina matatizo,
Watu wana matatizo,
Na hiyo ni fursa nzuri kwetu kuweza kupata chochote tunachotaka, kama tu tutatatua tatizo.
Watu wengi wamekuwa wakikazana kupata fedha, wakifikiria wanaipataje fedha.
Fedha ipo kwenye matatizo ya wengine, kadiri unavyoweza kutatua vizuri matatizo ya wengine, ndivyo unavyoweza kutengeneza kipato kikubwa.
Huu ndiyo msingi muhimu wa kuanzia, popote pale ulipo.
Kipato chako kinaendana na ukubwa wa tatizo unalotatua, na idadi ya wanaonufaika na suluhisho lako.
Kuongeza kipato, tatua tatizo kubwa zaidi au tatua tatizo linalowasumbua wengi zaidi.
Kwa vyovyote vile, tatua tatizo, kila wakati angalia ni wapi unaweza kutatua tatizo zaidi.
Je leo ni tatizo lipi unakwenda kutatua kwa wengine kupitia kazi na biashara yako?
Hapo ndipo pa kuianza kila siku yako, maana kunakupa mwongozo mzuri wa wapi uweke vipaumbele vyako.
Tatua tatizo, na tatizo la fedha litakuwa hadithi kwako.
Uwe na siku njema leo, na utatue matatizo ya wengine.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.
http://www.makirita.info