Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

Ni kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MUDA UPO WA KUTOSHA….
Malalamiko ya kila mtu ni kwamba hakuna muda, au muda hautoshi.
Wengi wamekuwa wakitaka kufanya makubwa, ila kusingizia kukosa muda.
Lakini mimi na wewe tunajua ya kwamba hakuna siku hata moja ambapo muda utaongezeka, hata dakika moja tu.
Hivyo kulalamika kwamba muda hautoshi, ni kupoteza muda, kwa sababu hakuna kitakachobadilika.
Hivyo mahali pazuri pa kuanzia ni kuanza na MUDA UPO WA KUTOSHA, kwa sababu kuanza hivi, tutaweza kuutumia vizuri muda ambao tunao kila siku.
Hatusemi tu hivyo kujiridhisha, bali ndiyo ukweli.
Ni kweli kwamba muda tunao wa kutosha,
Ila sisi wenyewe, tumekuwa tunatafuta namna ya kupoteza muda huu tulionao.
Tumekuwa tunatumia muda huu kufanya mambo ambayo siyo muhimu kwetu na wala hayana mchango wowote kwenye maisha yetu.
Ndiyo maana tunashangaa muda unakwenda na hatuoni nini tumefanya.
Muda upo wa kutosha iwapo utaupangilia vizuri,
Muda upo wa kutosha iwapo utaweka vipaumbele vyako,
Muda upo wa kutosha iwapo utakuwa mkali na muda wako,
Muda upo wa kutosha iwapo utasema HAPANA kwenye mengi.
Muda upo wa kutosna iwapo utaacha kufuatilia habari na kuzurura kwenye mitandao ya kijamii.
Muda upo wa kutosha iwapo utajua ni wapi unakwenda na ukawa na mipango ya kufika pale, na ukaifanyia kila siku.
Unapoona muda hautoshi, hebu kaa chini na angalia wapi unakosea, wapi unaupoteza, wapi huuthamini?
Katumie muda wako wa leo vizuri rafiki.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info