Biashara zote zenye mafanikio, zinajengwa kwenye vitu viwili vikuu;

  1. Bidhaa au huduma nzuri.
  2. Wateja wanaojirudia.

Unahitaji kuwa na bidhaa au huduma nzuri, siyo nzuri kwa sura, bali nzuri kwa uhitaji wa watu. Kile unachouza lazima kiwe kinatatua tatizo au kutimiza mahitaji ya wateja wako. Kiwe na thamani kwao inayowafanya kuwa tayari kutoa fedha zao, ambazo wamezipata kwa shida, kukinunua. Bila ya bidhaa au huduma nzuri, biashara haiwezi kuwepo.

Unahitaji kuwa na wateja wanaojirudia ili kuweza kutengeneza biashara yenye mafanikio. Kupata mteja anayekuja mara moja siyo ngumu, unaweza kuwahadaa watu wakaja kwenye biashara yako mara ya kwanza, ila mteja anaporudi tena na tena, ina maana ameikubali biashara, ina thamani kwake na hivyo kurudi tena. Wateja hawa ndiyo wanaokuletea mafanikio kwenye biashara yako, kwa sababu hutumii gharama kubwa kuwaleta tena, na wao wanawaleta wengine wengi zaidi.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujenga Biashara Kubwa Ya Wateja Wanaolipa Fedha Taslimu Na Siyo Mikopo.

Kitu muhimu kuelewa ni kwamba, vitu hivi viwili vinategemeana sana. Kwa sababu bila ya bidhaa au huduma bora, wateja hawawezi kurudi tena kwenye biashara yako. Hivyo lazima bidhaa au huduma unayotoa iwe bora, ili mteja anapokuja mara moja, ashawishike kuja tena mara nyingine na nyingine.

Bidhaa/huduma bora, na wateja wanaojirudia, kumbuka haya kila siku, na nguvu zako za kukuza biashara yako, zielekeze kwenye kuboresha unachotoa, na kujenga wateja ambao wanaiamini biashara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog