Huwezi kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa wewe peke yako. Unahitaji msaada wa watu wengine wengi ambao watafanyia kazi majukumu muhimu kwenye biashara yako. Hivyo kuajiri ni kitu ambacho kila mfanyabiashara akifikirie hata kama biashara ni ndogo kabisa.
Lakini pia kuajiri pekee hakutoshi kukuletea mafanikio kwenye biashara yako. Bali unahitaji kutoa mafunzo kwa wale unaowaajiri wakusaidie kwenye biashara yako. Watu unaowaajiri lazima wawe na uelewa wa kutosha kuhusu biashara yako, na pia wawe na uelewa wa kutosha kuhusu mafanikio ya biashara kwa ujumla.
Hata kama utaajiri watu ambao wana elimu kubwa, bado wanahitaji kupata mafunzo kuhusu biashara yako. Na kadiri siku zinavyokwenda, mambo yanabadilika na hivyo wanahitaji kujifunza mambo mapya ili kuweza kufanya maamuzi sahihi wanapokuwa kwenye biashara yako.
Kwa kusema hayo, ni muhimu sana mafunzo kwa wafanyakazi wako kuwa eneo muhimu la biashara yako. Litakunufaisha wewe kwenye biashara yako na pia litawanufaisha wafanyakazi wako kwenye maisha yao.
Zipo njia nyingi za kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa biashara yako. Hizi hapa ni tano muhimu unazopaswa kuzitumia kwenye kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa biashara yako.
- Kuwa na mwongozo wa majukumu ya kila eneo la biashara yako.
Ni muhimu uigawe biashara yako kwenye vitengo mbalimbali. Kama vile mauzo, masoko, huduma kwa wateja na kadhalika. Sasa unapoajiri mfanyakazi, unajua kabisa anakwenda kufanya kazi kwenye kitengo gani.
Sasa unahitaji kuwa na miongozo ya majukumu na ufanyaji kazi wa kila kitengo cha biashara yako. Kwenye miongozo hii mfanyakazi anajua wazi majukumu yake ni yapi na mambo muhimu kwake kuzingatia ni yapi. Miongozo hii inapaswa kuwa na matokeo ambayo mfanyakazi anategemewa kuzalisha.
Ni muhimu miongozo hii kuwa na mwongozo wa namna ya kufanya maamuzi kwenye nyakati za changamoto. Mwongozo huu unakuwa kitabu cha rejea cha mfanyakazi anapokuwa kwenye biashara yako.
Ni muhimu kila mfanyakazi kuwa na nakala ya mwongozo wa kazi na majukumu yake kwenye eneo lake la kazi katika biashara yako. Na pia kuhamasishwa kupitia mwongozo huo ili kuwa na uelewa mzuri juu ya majukumu yake.
- Kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wote kwa pamoja.
Hapa unahitaji kuwa na mafunzo mbalimbali yanayohusu biashara ambapo wafanyakazi wote wanahudhuria. Mafunzo haya unaweza kuandaa wewe mwenyewe kama mwenye biashara na kufundisha wewe au kualika wataalamu mbalimbali kufundisha. Katika mafunzo haya wafanyakazi wako wanapata mbinu za kuweza kufanya kazi zao kwa ubora zaidi.
Mafunzo haya yanapaswa kuwa ya mara kwa mara, labda kila baada ya miezi sita au kila mwaka. Mafunzo ya mara moja pekee hayatoshi, kwa sababu mambo wanayopaswa kujifunza ni mengi, na ili kueleweka kwa kitu, wanapaswa kukirudia mara nyingi mno.
- Mkutano na mfanyakazi mmoja mmoja.
Wewe kama mmiliki wa biashara, unahitaji kutengeneza mpango wa mafunzo wa kukutana na mfanyakazi mmoja mmoja kwa ngazi mbalimbali. Kama biashara yako ni ndogo na wafanyakazi ni wachache, unaweza kukutana na kila mmoja kwa wakati tofauti. Unahakikisha angalau kila mwezi unapata dakika 10 mpaka 15 za kukaa na kila mfanyakazi, kujua changamoto zake na kumpa mafunzo muhimu ya biashara.
Kama biashara yako ni kubwa na wafanyakazi ni wengi, basi unaweza kutengeneza mpango wa kukutana kwa ngazi mbalimbali. Kwa mfano wewe mmiliki au mkurugenzi unaweza kuwa unakutana na mameneja moja kwa moja, mameneja wao wanakutana na wale walioko chini yao, mmoja mmoja. Kwa njia hii unatengeneza mfumo mzuri wa mafunzo kwenye biashara yako.
SOMA; Tengeneza mfumo bora wa wafanyakazi kwenye biashara yako.
- Kila mfanyakazi kuwa na menta wake kwenye biashara.
Licha ya kuwa na mafunzo ya mmoja mmoja, unahitaji kutengeneza mfumo wa kuwa na menta kwenye biashara yako. Menta ni mtu ambaye ameshafanya kitu ambacho mtu mwingine anajifunza kufanya. Hivyo kwenye biashara yako kama una wafanyakazi ambao ni wazoefu, hawa wanaweza kuwa mamenta wa wafanyakazi wapya. Hivyo mfanyakazi mpya anapoajiriwa, anakabishiwa menta wake ambaye atakuwa anamwongoza katika kujifunza kazi zake. Menta huyu atakuwa naye karibu na kumsaidia kutatua changamoto zake.
Unahitaji kuwa makini kwenye hili la menta kwa sababu iwapo menta atakuwa na tabia zisizo nzuri, ataharibu wafanyakazi wengine pia. Hivyo hakikisha watu wanaoaminika ndiyo wanapewa jukumu la kuwa karibu na wale wanaojifunza kazi.
- Mpango binafsi wa kujisomea vitabu.
Hili ni muhimu lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa hawalizingatii. Unakuta kwenye biashara anaifunza kweli, anasoma vitabu na kuhudhuria mafunzo, lakini wafanyakazi wake hawapati maarifa yoyote.
Wewe kama mmiliki wa biashara, unahitaji kuhakikisha wafanyakazi wako wanapata maarifa sahihi, na anza kwa kuhakikisha wanajisomea. Unaweza kuanzisha maktaba ndogo kwenye eneo lako la biashara ambapo unakuwa na vitabu ambavyo wafanyakazi wako watajifunza mambo muhimu. Na kukawa na utaratibu wa angalau kila mfanyakazi kusoma kitabu kimoja kila mwezi. Kwa njia hii watajifunza mengi na itawasaidia katika ufanisi wao kwenye kazi zao.
Hizi ni njia ambazo mfanyabiashara yeyote anaweza kuzitumia kuhakikisha wasaidizi wake wanapata maarifa sahihi kwa ajili ya kuendesha majukumu yao ya kila siku. Ni muhimu uhakikishe wafanyakazi wako wanapata maarifa sahihi, na hili litakuwezesha wewe kupata matokeo mazuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
