Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Hii ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.


Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tunakwenda kutafakari kuhusu KUWA TAYARI KWA MIAKA MITANO…

Sijui ni nini kinatokea siku hizi, lakini watu hawana subira kabisa.
Watu hawana uvumilivu hata kidogo,
Wanataka kitu na wanakitaka sasa.
Kikichelewa wanaachana nacho na kukimbiza kitu kingine.
Hali hii imezalisha watu wengi ambao kila kukicha wanakimbizana na fursa mpya.
Hili limewapotezea watu muda na kujikuta wapo pale pale, hakuna hatua kubwa waliyopiga.

Kuondokana na hali hii rafiki, tumia sheria ya miaka mitano…
Kitu chochote unachoamua kufanya, basi hakikisha una uwezo wa kuweka miaka mitano.
Yaani hakikisha unakifanya kwa miaka mitano, kabla hujasema hakiwezekani na kuachana nacho au kuboresha zaidi.
Jitoe kwa miaka mitano, ukiweka juhudi kubwa sana ambazo hazijawahi kuwekwa.

Kama bado hujafanya kwa angalau miaka mitano, usijidanganye haiwezekani au haikifai wewe.
Kwa maana hii unahitaji kuwa makini unapofanya maamuzi ya kuanza kufanya kitu chochote kile.

Kuna sababu kwa nini hata viongozi wa kisiasa wanachaguliwa kila baada ya miaka mitano.
Chini ya miaka mitano hakuna kikubwa unaweza kufanya.
Chini ya miaka mitano bado unakuwa unajifunza.
Chini ya miaka mitano huwezi kusema imeshindikana,
Weka miaka hiyo mitano, ukiweka juhudi kubwa na maarifa, huku ukiendelea kujifunza na kuboresha zaidi.
Ndani ya miaka mitano, utaweza kujenga msingi imara sana wa mafanikio yako.

Ila ukiwa mtu wa kuruka ruka, utarukia kila kitu na utaona hakikufai.

Je upo tayari kufanya kwa miaka mitano?
Je kitu hicho kina nafasi ya kuwepo kwa miaka mitano ijayo?
Hayo ni maswali muhimu ya kujiuliza kabla hujaanza chochote.

Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info