Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MAONI YA WENGINE….
Katika kitu ambacho hakina uhaba, basi ni maoni ya wengine.
Watu wana maoni kwenye kila jambo,
Iwe wanalijua au hawalijui,
Iwe linawahusu au haliwahusu,
Wao wana maoni kwa namna wanavyojisikia wao wenyewe.
Hivyo kitu chochote ambacho utachagua kufanya kwenye maisha yako, watu watakuja na maoni yao.
Wapo ambao watasema wao ni wataalamu kwenye kile unachofanya na hivyo kutaka usikilize maoni yao.
Wapo ambao hawajawahi kufanya kama hicho lakini wana maoni ambayo wanataka yasikilizwe.
Wapo ambao wanajisikia tu kusema lolote kwa vile wameona wewe unafanya kitu.
Yoye haya ni maoni, ukweli halisi unaujua wewe mwenyewe,
Kwa sababu wewe ndiye uliyebeba ndoto kubwa ndani yako.
Kinachoshangaza ni namna watu wanavyopokea maoni ya wengine kama vile ndiyo ukweli.
Watu wamekuwa wakipokea maoni hayo na kuruhusu yavuruge kile ambacho wanafanya.
Kwa namna hii wanashindwa kupiga hatua.
Rafiki, unapopanga kufanya jambo, kwanza fanya utafiti wako. Jua ni yapi muhimu unapaswa kufanya, jua wapi pa kuzingatia. Jua changamoto zipi za kuvuka.
Halafu unapoingiam ingia kweli, ukiwa tayari kwa mapambano.
Maoni ya wengine yasikuyumbishe,
Wewe ndiye mwenye ndoto na maono makubwa,
Wewe ndiye unayejua unakokwenda,
Maoni ya wengine ni kelele ambazo ukizipa kipaumbele, hutakuja kufanya jambo lolote kubwa kwenye maisha yako.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki, nenda kaweke kazi ya kutosha.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info