Mtu yeyote, anaweza kujijengea mafanikio makubwa kabisa kwa kuanzia pale alipo sasa. 

Hii ina maana kwamba kama huna pa kuanzia kabisa, basi unaweza kuanzia chini kabisa, ukawaka juhudi na maarifa, ukawa mvumilivu na king’ang’anizi na ukaweka muda na hatimaye ukafikia mafanikio makubwa. Ni kitu ambacho kinawezekana, lakini siyo rahisi.



Na ugumu zaidi unaongezwa na mtazamo wa watu juu yetu, pale ambapo tunafikiria kwamba watu wengine watatuonaje pale wakituona tunafanya mambo ambayo yapo chini yetu. Labda tumesoma mpaka vyuo vikuu, na huna pa kuanzia, ukifikiria uanze biashara ndogo unaona watu watakudharau, na kukuona na elimu yako yote unafanya biashara kama hiyo! Kwa mtazamo huu wengi wanaona aibu, wanahofia na kuacha kabisa kufanya. 

Mwishowe wanabaki pale walipo, maisha yanazidi kuwa magumu zaidi.

Leo kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufanikiwa, tutakwenda kuangalia jinsi unavyoweza kuondokana na changamoto hii ya kuwa na aibu ya kuanzia chini kabisa. Kabla hatujaangalia hatua zipi za kuchukua, tusome maoni aliyotuandikia msomaji mwenzetu juu ya hili.

Nikitaka kuanzisha mradi mdogo naona aibu kubwa sana, nakomea kuahirisha tu. – Paschal C. T.

Ndugu Paschal na wasomaji wengine ambao mnapitia hali kama hii, kwanza kabisa niwape hongera kwa kuanza kufikiria kwamba njia pekee ya kutoka pale ulipo ni kuanzia pale ulipo, chini kabisa. Kwa kuanza tu kufikiria kuanza kidogo, maana yake umeshaondoka kwenye kundi kubwa la watu ambao wanasubiri siku mambo yatakuwa safi na maisha yao yatakuwa mazuri, bila ya wao kuchukua hatua.

Lakini mna changamoto hiyo ambayo mmeitengeneza au kuipokea wenyewe kutoka kwenye jamii inayowazunguka. Jamii imewafanya muamini kwamba, kwa kuanza kidogo basi nyie ni watu wa chini, watu msiofaa na watu ambao hamtafika popote. Mmepokea imani hiyo ya jamii kwa utiifu kabisa na kuchagua kuiishi.

Sasa leo nakwenda kuivunja kabisa imani hii na nakwenda kukupa uhuru wa kuchagua chochote kile unachotaka kufanya, bila ya aibu, bila ya hofu ya aina yoyote ile. Kwa uhuru huu, utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako kwa kuanzia chini kabisa.

Zingatia mambo yafuatayo ili kuondokana na aibu ya kuanzia chini.

1. Hakuna anayejali sana maisha yako zaidi yako mwenyewe.

Binadamu wote huwa tunafanya kosa moja moja kubwa sana, huwa tunaamini kama vile dunia nzima inatuangalia kwenye kila tunachofanya. Tunafikiri kwamba watu usiku wanakosa usingizi wakifikiria yale ambayo tunafanya au kutokufanya.

Ukweli ni kwamba watu wanafikiria zaidi maisha yao kuliko wanavyoyafikiria maisha yako. Watu usiku wanakosa usingizi kwa matatizo yao na siyo kuhusu wewe. Mtu anaweza kukuambia jambo la kukatisha tamaa, lakini usifikiri ndiyo atakufikiria wewe wakati wote, atarudi kufikiria matatizo yake.

Jipe uhuru wa kufanya kile ambacho unataka kufanya, kwa sababu kila mtu anahangaika na mambo yake. Hakuna atakayepoteza muda wake kukufuatilia wewe kwa kila unachofanya. Na atakayefanya hivyo basi jua yeye mwenyewe hana maisha ya maana kwake, na hivyo hana umuhimu wowote kwako.

2. Aibu ipo ndani ya akili yako.

Unaposema unaona aibu, jua kabisa hakuna kitu kilichotengenezwa ambacho ni aibu, bali aibu ipo ndani yako wewe. Ni fikra zako wewe ndiyo zinatengeneza hicho kitu unachosema ni aibu, na fikra hizo zinakuzuia wewe kuweza kuchukua hatua.

Aibu unayoona wala siyo aibu, bali ni uvivu unaokuzuia usichukue hatua. Kwa kuwa unajua kuanzia chini ni kazi kubwa, unajidanganya ni aibu kumbe ambacho unakimbia ni kazi. Kuwa tayari kuweka juhudi na aibu uliyonayo itakimbia yenyewe. 

3. Kama upo chini, huna hadhi yoyote, hivyo usijitengenezee vitu visivyokuwepo.

Kitu kingine ambacho kinakuzuia ni kujijengea hadhi ambayo wala huna. Unaweza kujidanganya kwamba kwa sababu una elimu kubwa basi una hadhi kubwa, sawa hadhi hiyo ni ndani yako, ila kwa duniani, kama huna unachofanya, huna hadhi yoyote. Hivyo kuacha kufanya jambo kwa sababu unaona siyo la hadhi yako, au litakushushia hadhi yako, hebu tuambie ni hadhi ipi hiyo?

Kama hakuna unachofanya hadhi ipo wapi, kama upo chini kabisa unahesabu vipi hadhi yako? Usikubali akili yako iendelee kukudanganya kwamba una hadhi wakati huna pa kuanzia. Anza sasa na utatengeneza hadhi yako. Kama hujaanza huna hadhi yoyote hivyo epuka kujidanganya.

4. Usipochukua hatua sasa utabaki hapo ulipo.

Utaendelea kubaki hapo ulipo sasa, mpaka pale utakapoamua kuchukua hatua. Na mbaya zaidi, hakuna atakayekuchukulia wewe hatua, huo ni mzigo wake mwenyewe, na kama unavyojua, kila mtu atabeba mzigo wake.

Kama unataka kuendelea kuwa chini, kuendelea kunyanyasika na kujiona hufai, basi endelea kubaki hapo ulipo, ukijidanganya kwamba ukianzia chini watu watakudharau au kukucheka.

Hakuna mtu yeyote anayeweza kukudharau, na hata akifanya hivyo haliwezi kukusumbua mpaka pale wewe mwenyewe utakapoamua kupokea dharau hizo na kuzifanya sehemu ya maisha yako. Lakini kama utakuwa bize kufanya yako, wala hata hutajua watu wanasema nini.

5. Tatizo siyo unaanzia wapi, bali wapi unapoelekea.

Kuanzia chini siyo shida, kama una ndoto na maono makubwa ya maisha yako. Hivyo kuanza chini leo, haimaanishi utaendelea kuwa chini daima. Kila mtu ambaye yupo juu leo alianzia chini kama wewe ulipo.

Soma hadithi za watu waliofanikiwa, tafuta watu unawafahamu ambao wamepiga hatua. 

Kaa nao, jifunze kutoka kwao na utaona karibu kila mtu kuna wakati alianzia chini kabisa. 

Alipambana na kuweza kufika pale alipo sasa. Hivyo kama na wewe utapambana, hutabaki hapo ulipo.

6. Tenga miaka michache ya kuchekwa na kudhihakiwa, na utaishi miaka mingi ya heshima kubwa.

Basi nikubaliane na wewe kwamba labda kweli marafiki zako watakucheka na kukudharau. Basi amua kutenga miaka michache ya kuchekwa na kudharauliwa, kubali kutenga muda huo kuweka juhudi kubwa. Lakini baada ya hapo, wote waliokuwa wanakucheka, watakudharau. Baada ya kuwa umeweka juhudi kubwa na kutengeneza msingi mzuri, utajikuta unawaajiri wale ambao walikuwa wanakuambia umepotea. 

Ndivyo dunia ilivyo, siku zote wale wanaodharauliwa ndiyo huja kufanya makubwa. 

Naamini na wewe utakuwa mmoja wa watu hawa.

Neno la mwisho kwako rafiki yangu, anzia hapo ulipo, angalia kile unaweza kufanya sasa na kifanye. Na tena usifanye kitu kimoja, fanya vitu vingi. Anza biashara ndogo, kama kuna mahali unaweza kujitolea fanya hivyo, kama unaweza kuwasaidia watu fanya hivyo, angalia kila fursa iliyopo mbele yako ya kuweza kuongeza thamani kwa watu. Kama unaweza kupata kazi ya kuuza bidhaa na huduma za wengine kwa kamisheni, tumia fursa hiyo. Wakati huo endelea kujifunza na kujijengea uwezo wa kibiashara na kufanya makubwa. Endelea kuitengeneza ndoto ya maisha yako. Na epuka kabisa hali zozote ambazo zitakurudisha nyuma. Epuka marafiki wanaokukatisha tamaa na kukurudisha nyuma. Epuka mambo yote ambayo yanakupotezea wewe muda wako. Na kwa kuanzia hapo ulipo sasa, utaweza kufika mbali sana, kama utaweka juhudi, hutokata tamaa na ukawa mvumilivu.

Hakuna anayekuzuia wewe kufanikiwa zaidi yako wewe mwenyewe. Adui yako mkubwa ni wewe mwenyewe. Pambana na adui huyo kwa kuchukua hatua sasa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog