Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Umeianzaje siku hii nzuri sana ya leo.
Hongera kwa nafasi hii nyingine, ambapo ni fursa nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA utakaotuwezesha kufanya makubwa.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UPO KWENYE NJIA SAHIHI…
Kwanza kabisa, safari ya mafanikio siyo rahisi, ina changamoto na vikwazo, inahitaji muda na uvumilivu. Inahitaji kazi.
Lakini wakati wewe unakutana na hayo, ni rahisi kuona wengine kama vile mambo ni rahisi zaidi kwao.
Unawaona wakiwa na furaha, unaona kila kitu wanafanikiwa, huwaoni wakilalamika, na hapo unajishawishi kwamba, wao wapo kwenye njia sahihi ila wewe haupo kwenye njia sahihi.
Na hapo ndipo unakuwa umejipa uongo mkubwa na wa kipekee.
Kwa sababu unaona watu wanafuraha kwenye kile wanafanya, kwa sababu huwaoni wakilalamika, haimaanishi ni rahisi wanachofanya. Mara nyingi watu hao wamekikubali na wanaweka juhudi, kwa sababu wanajua kufanya kinyume na hivyo ni kupoteza muda.
Huenda ukipewa nafasi ya hao wengine unaoona wapo vizuri kuliko wewe, ukaishindwa kabisa.
Kwa hiyo rafiki yangu, nakukumbusha ya kwamba, hapo ulipo, upo kwenye njia sahihi, kama tayari umeshaitengeneza ndoto yako na unaifanyia kazi.
Na hata kama bado hujatengeneza ndoto yako, basi kwa sasa angalau upo sehemu sahihi.
Kuruka ruka kwa kujaribu kila unachoona wengine wanafanya, hakutakusaidia wewe kwa namna yoyote ile.
Usisahau pia kwamba nyasi za ngapo ya pili huwa zinaonekana ni za kijani kuliko za pale ulipo, ukizisogolea karibu, unagundua siyo za kijani kama zilivyoonekana kwa mbali.
Upo kwenye njia sahihi, angalau kwa sasa.
Unachohitaji ni kukubali pale ulipo, kuweka juhudi kubwa, kuwa mvumilivu na kujua unahitaji muda kufika pale unataka kufika.
Na waache wengine wafanye yao.
Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info