Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUACHA KUJIDANGANYA….
Nafikiri moja ya vikwazo vikuu kwa wengi kufanikiwa ni kujidanganya, yaani mtu mwenyewe, unajitengenezea uongo ambao unauishi wewe kwenyewe.
Na uongo huu unakuwa mgumu kuuvunja kwa sababu inafika mahali mtu anasahau kama ni uongo.
Baada ya kuishi uongo muda mrefu, unaamini kwamba ni ukweli na hii inafanya kazi ya kuuvunja kuwa kubwa zaidi.
Yapo mengi ambayo watu wamekuwa wanajidanganya mpaka wakaishia kuamini, kwa mfano;
Kuajiriwa ni usalama wa kipato, kitu ambacho siyo kweli, ni kujidanganya kulikopitiliza. Na wengi walioamini hilo wamekuwa wanajiwekea ukomo kwenye uwezo wao wa kutengeneza kipato.
Au kuanza biashara ni mpaka uwe na mtaji mkubwa, kitu ambacho siyo kweli lakini kimewazuia wengi kuingia kwenye biashara.
Au kuacha kufuatilia kila habari utapitwa na mazuri, uongo ambao umewafanya wengi kuendelea kupoteza muda mzuri na wa kipekee uliopo mbele yao.
Haya ni machache mno kati ya mengi ambayo watu wanajidanganya.
Sasa kazi yako leo rafiki yangu ni hii,
Tafakari kila unachoamini kwenye maisha yako, na jiulize je huo ni ukweli au ni uongo uliojitengenezea muda mrefu mpaka sasa unauamini?
Kila jambo lipime hivyo, kwa kuangalia uhakika wake na hata kinyume chake.
Hii itakusaidia kuvunja imani nyingi ambazo zinakurudisha nyuma.
Fanya zoezi hili ili kuacha kujidanganya.
Uwe na siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info