Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera sana kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu, kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Ni kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tunakwenda kutafakari kuhusu UKOMO WA KIPATO….
Ni jambo la kushangaza, hata kwenye ulimwengu wa sasa, ambapo zipo fursa na nafasi nyingi za kutengeneza kipato, bado watu wanakubali kuwa na ukomo wa kipato.
Kuwa na ukomo wa kipato ni pale wewe mwenyewe, unapokubali watu wengine wa kupangie ni kiasi gani unastahili kulipwa, na wewe unakubaliana nao.
Unapokuwa kwenye ajira unakuwa na ukomo wa kipato, maana mwajiri ndiye mwenye maamuzi ya mwisho akulipe kiasi gani.
Ukiwa kwenye biashara ambayo mteja ni mmoja au wachache, kadhalika una ukomo wa kipati, hata kama ananunua kwa ukubwa kiasi gani.
Unapokuwa kwenye biashara ambayo inatoa bidhaa na huduma zile zile, kwa kiwango kile kile, eneo lile lile na kwa watu wale wale, umeamua kujitengenezea ukomo wa kipato.
Inaonekana kama sisi binadamu ni viumbe ambao huwa hatupendi kujisumbua,
Tukishapata sehemu ambayo inatupa kila tunachohitaji kwa wakati huo, tunasahau kabisa mahitaji yetu ya mbele na kuridhika.
Tukisahau kwamba, mahitaji yetu ya mbele ni makubwa kuliko tulichokubali awali.
Ili kufanikiwa, lazima tuondoe kila aina ya ukomo kwenye maisha yetu.
Na ukomo wa kwanza kuuvunja ni ukomo wa kipato.
Huu ndiyo mbaya na unaosumbua wengi.
Tumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako, na mazingira yanayokuzunguka kuhakikisha unaongera kipato chako kila wakati.
Kwa mfano,
Hakuna sheria inayosema mtu ukishaajiriwa hupaswi kufanya kitu kingine chochote ila ajira, ni mazoea tu.
Hakuna sheria inayosema mtu ukishafika miaka 60 huruhusiwi kufanya kazi zako binafsi, ni mazoea tu.
Hakuna sheria inayosema biashara ikishajiendesha kwa faida basi umefikia kilele, ni kujiridhisha tu.
Ni muhimu uanze kuiangalia kesho na ukumbuke kinachokuvusha leo, kesho kinaweza kukuangusha. Na kuwa na ukomo wa kipato, ni kitu hatari sana kwenye maisha yako.
Uwe na siku njeka rafiki, anza kuvunja ukomo wowote uliouruhusu kwenye maisha yako leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info