Pamoja na hayo, uongozi siyo rahisi, hasa nafasi ya uongozi inapokuwa kubwa. Kuna wakati kiongozi anajikuta njia panga, kwa kuwa hatua anazotaka kuchukua zitakuwa na manufaa, lakini pia zitawaumiza wengi.
Viongozi wamekuwa wanashindwa, wamekuwa wanapambana na wamekuwa wanafanikiwa. Katika kitabu hichi mafundisho ya viongozi wawili, Warren Bennis na
Steven Sample, yamewekwa pamoja kwa ajili ya kutuandaa sisi kama viongozi kwa maeneo mbalimbali ya maisha yetu.
Karibu tujifunze kwa pamoja mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza kuwa viongozi wenye mafanikio.
1. Uwezo wa kuvuka kushindwa ndiyo unatengeneza viongozi wenye mafanikio.
Siyo kila mtu bora anaweza kuwa kiongozi, na siyo kila kiongozi anakuwa mtu bora.
Uongozi hautokani tu na vipaji, uwezo, umaarufu au bahati. Uongozi unazaliwa pale mtu anapoweza kuvuka kushindwa na changamoto. Vikwazo na changamoto vipo kwenye maisha ya kila mtu, wale wanaoweza kuvivuka wanakuwa viongozi bora.
2. Watu wanapenda makubwa, lakini hawapendi kushindwa.
Kila mtu anapenda kufanya makubwa, kila mtu anapenda kuwa maarufu, lakini inapokuja wazo la kushindwa, wengi husita kuchukua hatua. Na wale wachache wanaothubutu kuanza, wanapokutana na kushindwa, wengi huishia hapo. Hii ndiyo sababu viongozi wanakuwa wachache kwenye jamii yoyote.
3. Uongozi ni kucheza a moto.
Moto ni kitu kizuri, iwapo kitatumiwa vizuri. Lakini ukitumiwa vibaya, moto ni silaha hatari na inayoweza kuangamiza vitu vingi. Uongozi ni sawa na kucheza na moto, unaweza kufanya makubwa, lakini pia ukikosea, unatengeneza madhara makubwa.
4. Hakuna kanuni rahisi.
Kwenye uongozi, hakuna kanuni rahisi, hakuna njia rahisi ya kufuata. Meneja anajua kanuni za kufuata, na anazifuata hizo wakati wote. Kiongozi ni tofauti, kiongozi anakutana na changamoto ambazo ni ngumu na zinamhitaji yeye kufanya maamuzi.
Maamuzi ambayo yanaweza kuwa bora na kuwasaidia wengi, au yakawa hovyo na yakawaumiza wengi.
Hata kanuni ambazo viongozi wengine wametumia wakafanikiwa hazifai kila mahali na kila wakati. Hata uzoefu wa kiongozi mwenyewe haufai kila mahali na kila wakati. Kila wakati kiongozi anapaswa kuja na majibu yanayoendana na hali na wakati huo.
5. Kiongozi lazima awe vizuri kwenye ugumu na urahisi.
Kiongozi anahitaji kuweza kuelewa vitu vigumu, na kuweza kuvielezea au kuvifanyia kazi kwa urahisi kwa wale ambao anawaongoza. Kutumia vitu vigumu kwa wale unaowaongoa, kutaongeza changamoto za uongozi.
6. Msukumo wa uongozi unasaidia.
Kuna watu ambao wanachukua nafasi za uongozi kwa sababu ndani yao wanapata msukumo wa kuwaongoza wengine, hawa wanakuwa viongozi bora na kuweza kuvuka changamoto nyingi.
Kuna watu ambao wanachukua nafasi za uongozi, ili kujenga majina yao, ili kupata umaarufu au kupata upendeleo kwenye nafasi fulani fulani, hawa huwa viongozi wabovu na hushindwa kabisa.
7. Viongozi wazuri huanza kujisimamia wenyewe.
Viongozi bora huanza kujisimamia wao wenyewe kabla hawajasimamia watu wengine.
Hujua nguvu zao ziko wapi na udhaifu wao uko wapi. Hujua vipaji vyao na uwezo wao na namna ya kutumia katika kile wanachofanya. Kwa njia hii wanakuwa bora wao na kuweza kuwaongoza wengine vizuri.
8. Sheria ya 70/30 kwenye uongozi.
Matumizi ya muda wa kiongozi yanafuata sheria ya 70/30. Asilimia 70 ya muda wa kiongozi anautumia kwa mambo madogo madogo na yanayohusu watu wengine. Asilimia
30 ya muda wake ndiyo anaitumia kwenye mambo muhimu na makubwa.
Kwenda kinyume na sheria hiyo, hasa kuongeza muda kwenye mambo makubwa na kudharau madogo, hutengeneza matatizo makubwa na kupelekea kiongozi kushindwa.
Mambo madogo madogo ni muhimu sana kwenye uongozi.
9. Uongozi unahitaji kiasi, na kujua wapi pa kuishia.
Dunia imewahi kupata viongozi waliokuwa wakubwa sana, lakini ukubwa wao ukawaangamiza. Hii inatokana na tabia ya binadamu ya kukosa kiasi, kiongozi anapambana na kufanya makubwa, lakini anaendelea kutaka makubwa zaidi, hata kama hayana manufaa tena kwake.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa watawala waliokuwa wakikuza tawala zao, walikwenda mbali zaidi na mwishowe kujikuta wanaanguka vibaya. Kama kiongozi unahitaji kuwa na kiasi na kujua wapo pa kuishia. Usikimbilie au kupigania kila kitu.
10. Kiongozi anahitaji kuwa na maadili yake, lakini pia awe tayari kuyavunja.
Kiongozi bora anapaswa kuwa na maadili yake, huu ni msimamo wake kwenye mambo gani anafanya na yapi hafanyi. Maadili ndiyo yanayomjenga kiongozi.
Lakini pia kwenye uongozi, kuna wakati inafika ambapo kiongozi anapaswa kuvunja maadili yake. Kuna wakati itampasa kufanya kitu ambacho amejiwekea kutokufanya. Na hapo ndipo uongozi unapokuwa changamoto kwa wengi.
Kuna wakati kiongozi mzuri anapaswa kufanya mabaya ili kuondokana na changamoto kubwa inayosumbua.
11. Kiongozi lazima awe na mawazo huru.
Jamii yetu inakazana kufanya kitu kimoja, kuhakikisha kila mtu anafanya kile ambacho kila mtu anafanya. Kuna mambo mengi yanayotulazimisha kuwa kama wengine. Vyombo vya habari na propaganda mbalimbali zinatutengenezea namna ya kufikiri.
Kiongozi bora lazima aweze kuvuka mtego huo, anahitaji kuwa na mawazo huru, kuweza kufikiria yeye kama yeye na siyo kwa propaganda zinazotengenezwa au habari zinazovuma.
12. Habari ni sumu kwa viongozi wengi.
Vyombo vya habari vimekuwa vikitoa habari ambazo nyingi siyo kweli kwa asilimia kubwa. Kiongozi kutegemea habari za aina hii kutampelekea yeye kufanya maamuzi yasiyo sahihi.
Kiongozi anapaswa kuwa makini sana na habari na vyombo vya habari. Kutokuvitegemea na kuviamini sana. Badala yake kujielimisha kwenye kila jambo analofanya.
Kiongozi anaweza kwenda vizuri hata kama hatafuatilia habari moja kwa moja. Kwa sababu habari kama ni muhimu ataisikia kwa wengine, na habari nyingi hazina umuhimu mkubwa.
13. Kiongozi lazima asome vitabu.
Kiongozi ambaye hasomi vitabu, hajui anachofanya. Kupitia vitabu kiongozi anajielimisha, na pia anaweza kutengeneza mawazo huru. Vitabu vimeandikwa kwa tafiti na uchunguzi wa kina, tofauti na habari ambazo zinapoteza thamani kwa wakati.
Kiongozi anapaswa kusoma vitabu ambavyo vimedhibitika kuwa bora, kwa kuendelea kuwepo kwa miaka mingi. Kama kitabu kimeandikwa miaka 100 iliyopita na bado watu wanakisoma, hicho ni kitabu bora kwa kiongozi kusoma.
14. Vitabu ambavyo kila kiongozi anapaswa kusoma.
Pamoja na uwepo wa vitabu vingi, kuna vitabu ambavyo kila kiongozi anapaswa kuvisoma. Vitabu hivi vina mafunzo mazuri sana kuhusu uongozi na hata watu kwa ujumla. Vitabu hivyo ni;
i/. The Prince kilichoandikwa na Nocola Machiavelli, hichi kina miaka zaidi ya 400 na bado ni muhimu kwa viongozi.
ii/. Hadithi za viongozi wakubwa wa nne kwenye biblia ambao ni Musa (kitabu cha kutoka), Daudi (kitabu cha Samweli), Yesu (kitabu cha Matayo) na Paulo (kitabu cha Matendo).
iii/. Republic kilichoandikwa na Plato, hichi kina zaidi ya miaka 2000.
iv/. Hamlet kilichoandikwa na Shakespare.
v/. Antigone kilichoandikwa na Sophocles
vi/. The devine comedy kilichoandikwa na Dante.
15. Watu hawajabadilika sana.
Moja ya makosa ambayo watu hufanya kwenye kufikiri ni kuamini kwamba siku hizi watu wamebadilika sana. Lakini ukweli tabia za watu ni zile zile, tangu zama za mawe mpaka zama hizi za viwanda na taarifa. Mahitaji ya watu ni yale yale, hofu za watu ni zile zile. Kwa kiongozi kujua vizuri tabia za watu, kunamsaidia kuweza kuchukua hatua nzuri.
Kwa kusoma vitabu vya zamani ambavyo mpaka sasa vipo, kunampa kiongozi nafasi nzuri ya kujifunza na kuchukua hatua.
16. Nenda kule ambapo washindani wako hawaendi.
Kuna mambo mengi sana ya kufanya, na muda ni mchache. Viongozi wengi hujikuta njia panda wafanye kipi na waache kipi. Katika kutatua hili, wanaweza kuchagua kwenda kule ambapo wengi hawaendi, kufanya kile ambacho wengine hawataki kufanya. Na hata kwenye kusoma, soma kile ambacho wengine hawasomi. Hii inamweka kiongozi mbele ya wengi na hivyo kuweza kufanikiwa.
17. Demokrasia siyo mfumo bora wa uongozi, ila ni mfumo mzuri ukilinganisha na mifumo mingine.
Demokrasia imekuwa na changamoto nyingi kwenye uongozi. Demokrasia imekuwa inachelewesha mambo kwa sababu kukubaliana kwenye jambo mpaka kila mtu asikilizwe. Wengi wamekuwa wakiona kuna wakati udikteta kidogo unahitajika. Lakini changamoto ni kwamba, tabia za binadamu ni za kushangaza. Mtu anapopata nafasi ya kufanya kitu bila ya kuhojiwa, huwa anatumia nafasi hiyo pia kujinufaisha yeye mwenyewe. Ndiyo maana mambo yanayoendeshwa kidikteta, hata kama yatakuwa mazuri, bado kuna namna watu wanajinufaisha zaidi. Hivyo ukilinganisha na mifumo mingine ya uongozi, mfumo wa demokrasia ni mzuri, lakini bado una changamoto zake.
18. Demokrasia inafanya kazi vizuri inapoeleweka vizuri.
Ili demokrasia iwe bora, inahitajika kueleweka vizuri na wote wanaohusika. Watu waelewe kwamba kwenye demokrasia huwezi kupata kila unachotaka kwa namna unavyotaka wewe. Kila mtu ana maoni tofuti na kukaa pamoja lazima kila mmoja akubali kupata na kupoteza pia.
19. Kushindwa kwa kiongozi ni kubaya zaidi.
Pamoja na kwamba kila mtu huwa anashindwa kwenye maisha, katika mambo mbalimbali, kushindwa kwa kiongozi ni kubaya zaidi kwa sababu kila mtu anaona.
Kushindwa kwa kiongozi kunakuwa hadharani na hii ndiyo inawafanya wengi kutokupenda kuwa viongozi. Kiongozi anaonekana na kila mtu na anafuatiliwa kwa kila jambo. Kosa lolote analofanya, linaonekana na kila mtu.
20. Kuepuka kushindwa, kunawafanya viongozi kushindwa zaidi.
Kwa kuwa kushindwa kwa viongozi kunaonekana na kila mtu, viongozi wengi hujitahidi kuwa makini ili wasishindwe. Katika kuwa kwao makini hukazana kuwa wakamilifu na hivyo kuogopa kufanya vitu vinavyoweza kuwapelekea kushindwa. Kwa kuacha kufanya vitu hivyo, ndiyo wanashindwa zaidi.
Kama kiongozi jua kwamba utashindwa, na kushindwa kwako kutakuwa wazi kwa kila mtu. Badala ya kuwa mwangalifu, ni muhimu kujenga msingi mzuri wa namna ya kufanya mambo yako, siyo kuepuka kushindwa, bali unaposhindwa ujue mapema na uweze kuchukua hatua ya kurekebisha.
Kama kiongozi, unahitaji sana kuwa na mawazo huru na uelewa wa mambo utakaokuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwenye nyakati mbalimbali unazopitia kwenye uongozi wako.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
UCHAMBUZI WA KITABU; The Art And Adventure Of Leadership (Jifunze Kushindwa, Kuvumilia Na Kufanikiwa Kama Kiongozi)
Uongozi ni nafasi ambayo kila mwanadamu anaipata kwa kuweza kutoa mawazo, ndoto na maono yake kwa wengine, ili kuweza kuchukua hatua ya kufanya mambo kuwa bora zaidi. Uongozi ni kitu ambacho kimekuwa na mjadala mpana, kuhusu viongozi wazuri na viongozi wabaya. Kipi kinamfanya mtu kuwa kiongozi bora na kipi kinamfanya kuwa kiongozi mbaya.
