Makosa ya binadamu ni yale yale, miaka nenda miaka rudi.

Mwaka 2000 palitokea mgogoro wa kiuchumi, hasa nchini marekani, ambapo hisa za makampuni ya mtandao wa intaneti zilishuka ghafla. Hali hii ilipelekea wengi ambao walikuwa wanaonekana mamilionea, kufilisika kabisa. Kilichopelekea hali hii ni kuvuma kwa habari za biashara ya intaneti, kila mtu akaanza kuona ni fursa, kila mtu akawa anaizungumzia, ikakua haraka kama pulizo linalojazwa upepo na hatimaye kupasuka.

Baada ya anguko hili, wengi wakajifunza, wakaona biashara ya intaneti siyo ya kutegemewa sana, basi wakaangalia kipi cha kuegemewa? Ikaonekana ni mali, yaani real estate. Basi hiyo ndiyo ikawa habari na fursa, kila mtu akakimbilia kununua au kukopa nyumba. Mabenki yakakopesha mpaka wasio na sifa. Matokeo yake mwaka 2008 likatokea anguko kubwa la kiuchumi, ambalo safari hii lilihusisha uwekezaji kwenye mali. Na hili lilikuwa baya zaidi kwa sababu liliathiri mpaka mabenki makubwa, kutokana na mikopo mikubwa iliyotolewa.

Na huo siyo mwisho, yapo maanguko mengine yatakayokuja, kwa sababu ni tabia yetu binadamu, kukimbilia kile ambacho ni rahisi.

Ukiacha maanguko hayo makubwa ya kiuchumi, zipo changamoto ndogo ndogo za kiuchumi ambazo watu wanakutana nazo kila siku kwa dhana hiyo. Kwa mfano kama mwaka huu nyanya zimekuwa adimu, na nyanya zikauzwa bei kali, basi tegemea mwaka unaofuata nyanya zitakuwa nyingi na bei yake kuwa ya chini kabisa. Kwa sababu watu wanapoona kitu ni adimu, wote hukimbilia kukifanya, kinakuwa fursa, na hapo kila mtu anazungumzia fursa hiyo na kuwapoteza wengi.

Ndiyo maana nasema, kama fursa inazungumzwa na kila mtu, basi umeshachelewa. Umeshachelewa kwa sababu wenzako wengi watakuwa wameshachukua hatua mapema, na wao ndiyo watanufaika zaidi.

Kila mtu anaposema kitu fulani kinalipa, na wakakimbilia kufanya, jipunguzie matatizo kwa kutokufanya kitu hicho, kwa sababu kitu kikishafanywa na wengine hakilipi tena.

Ni sheria ya uchumi kwamba uhaba ndiyo unaotengeneza thamani.

SOMA; Mambo Matano(05) Ya Kufanya Pale Unapokuwa Umekwama.

Sasa ufanyeje rafiki?

Kuwa mbele ya kundi, ona fursa kabla wengine hawajaziona, na chukua hatua mapema. Ukiwa mtu wa kujifunza, mtu wa kudadisi, mtu wa kubuni na kufanyia kazi mawazo mapya, lazima utaziona fursa nyingi kabla ya wengine. Utazifanyia kazi na mpaka watu wanapokuja kugundua ni fursa, wewe ndiyo utakuwa unanufaika zaidi.

Lakini pia sisemi uwe mcheyo na kujificha na fursa zako mwenyewe, usiwe tu kama kundi kubwa la watu ambao wanapenda mteremko, wasiopenda kufikiri na wanaotafuta njia ya mkato.

Zione fursa kabla ya wengine na chukua hatua, na ukishasikia kila mtu anazungumzia fursa fulani, jipunguzie matatizo kwa kuachana nayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog