Mahusiano yoyote bora na ya aina yoyote ile, yamejengwa kwenye msingi wa utegemezi. Pale ambapo kila mmoja anamtegemea mwenzake kwa kitu fulani, ndipo umuhimu wa kila mmoja unapoonekana na mahusiano kuwa bora, pale ambapo kila mtu anatimiza kile anachotegemewa.

Kwenye biashara pia hali ni hiyo, pale mteja na mfanyabiashara wanapokuwa na utegemezi wa kila mmoja, ndipo mahusiano bora ya kibiashara yanapojengwa.

Hakuna ubishi kwamba biashara yako inawategemea sana wateja, walipie huduma au bidhaa ili uweze kupata fedha ya kuendesha biashara na maisha yako pia. Kama ingekuwa huwategemei wateja, usingeiita biashara, bali ingekuwa kituo cha misaada au namna nyingine yoyote.

Hivyo upande mmoja wa shilingi tayari upo na una utegemezi.

Upande wa pili ili kukamilisha mahusiano mazuri, ni upande wa mteja. Je yeye mteja anakutegemea wewe au biashara yako kwa nini? Ni kipi ambacho kinamfanya mteja aendelee kuja kwenye biashara yako? Kwa sababu bila ya utegemezi, hakuna kitakachomsukuma kuja na hutaweza kujenga wateja waaminifu wa biashara yako.

SOMA; Ushindi Kwa Mteja Wako…

Tengeneza utegemezi wa wateja wako kwa kujua tatizo lao hasa ni lipi, jua mahitaji yao makuu ni yapi na pia jua mategemeo yao makubwa ni yapi. Hapo sasa unaweza kujenga biashara ambayo inakamata kila eneo hilo la wateja wako. Inatatua matatizo yao, inawapa mahitaji yao na inafikia matarajio yao.

Chini ya hapo utamwacha mteja akifikiria aende wapi ili akapate kile anachotaka kwa uhakika zaidi, na hivyo utampoteza.

Usikubali kuendesha biashara ambayo hakuna kitu chochote mteja anategemea kwako, na ninaposema anategemea kwako maana yake hawezi kupata sehemu nyingine yoyote, ni kwako tu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog