Habari za leo rafiki?

Nilianza kuandika kwenye blogu mbalimbali tangu mwaka 2012, ilipofika mwaka 2013 nilianzisha blog ya AMKA MTANZANIA, ambayo imeweza kuwafikia na kuwasaidia wengi. Najua unaijua na ndiyo maana mpaka sasa upo hapa.



Siku za mwanzo za AMKA MTANZANIA zilikuwa siku ngumu zaidi, kwa sababu wasomaji walikuwa wachache, wanaokubali kazi zile walikuwa wanakaa kimya tu, ila wasiokubali walikuwa wanapinga na kukatisha tamaa waziwazi. Isingekuwa ni kitu nilichochagua kufanya maisha yangu yote, huenda nisingefika mbali. Na wengi waliokuwa wanaanza blog za mafunzo kipindi kile, sijui hata wako wapi, waliishia njiani.

Mwaka 2014 nikaona bado wapo watu wanataka zaidi kutoka kwangu. Wanasoma AMKA MTANZANIA kila siku lakini bado wana kiu ya maarifa. Hapo nikapata wazo la kuanzisha KISIMA CHA MAARIFA, ambapo wale ambao wanasoma AMKA MTANZANIA, lakini wanataka zaidi, basi waweze kujiunga kwa kulipa gharama kidogo, wakati ule ilikuwa ni shilingi elfu 10 tu, na unalipa mara moja basi. Kipindi hicho nilikuwa naiendesha blog hiyo ya KISIMA CHA MAARIFA bure, na kama ujuavyo, chochote cha bure kina ukomo. Na ukomo ulikuwa ni watu 100 tu, huwezi kuwa na wasomaji zaidi ya hapo.

Mwaka huo huo 2014 wasomaji walifika 100 na hivyo ikawa hakuna tena namna ya kuongeza wapya. Hapo ndipo nilifikiria kuwekeza fedha zaidi ili kuweza kuruhusu watu wengi zaidi kujiunga. Na kwa kuwa fedha za kuweka mtandao wowote hewani zinalipwa kila mwaka, basi mpango wa kulipia ukabadilika kutoka ada ya mara moja mpaka ada ya kila mwaka, kutoka elfu 10 mpaka elfu 30 na baadaye elfu 50.

Mabadiliko yote haya yamekuwa yanakutana na changamoto nyingi kutoka kwa wasomaji. Lakini nimekuwa nashukuru mara zote, tunazitatua na mambo yanakwenda vizuri.

Sasa hivi tunaelekea mwisho kabisa wa kujiunga na semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ambayo nitaiendesha kupitia KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya mtandao. 

Hivyo kushiriki semina hii unapaswa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, kwa kulipa ada ambayo ni shilingi elfu 50 kwa mwaka. Sasa ninapotoa taarifa hizi wapo ambao wananiandikia kwamba hawataweza kushiriki kwa sababu kwa sasa hawapo vizuri kifedha. Na mimi nimekuwa nawajibu kwa kuwapa njia za kuendelea kujifunza mpaka pale watakapokuwa vizuri kifedha ndiyo wakaribie kwenye KISIMA CHA MAARIFA. 

Kwa sababu hichi ni kitu ambacho natarajia kukifanya maisha yangu yote, hivyo yapo mengi tutaendelea kujifunza pamoja.

Lakini wapo watu ambao wananiandikia kwamba KAMA LENGO LANGU NI KUWASAIDIA WATU, KWA NINI NINAWEKA GHARAMA ZA KUSHIRIKI MAFUNZO HAYA? Kwa nini nisiwasaidie bure halafu wayatumie maarifa hayo kuboresha maisha yao?

Ni hoja nzuri sana hiyo, lakini pia ni hoja ambayo imekaa kwa kitu ambacho nimewahi kuandika siku za nyuma kwamba KUNA WATU HAWANA SHUKRANI.

Sasa leo nimeona nichukue nafasi hii kuwaelewesha vizuri wale wenye hoja hii ya kwamba kwa nini niwatoze fedha kama lengo langu ni kuwasaidia watu.

Nikiri kweli kwamba lengo langu kubwa, kwa chochote ninachofanya, ni kuwasaidia watu. Kuona watu wanafanya maamuzi bora yanayowawezesha kufanikiwa. Kuona watu wanaepuka makosa yanayogharimu biashara zao. Kuona watu wakiwa na nidhamu nzuri ya fedha, wakiweka akiba, wakiwekeza, wakianzisha biashara na hatimaye kufikia uhuru wa kifedha.

Na kwa nafasi kubwa kabisa, hayo yote nayafanya kwa sehemu kubwa bure kabisa. 

Kupitia makala ninazoandika kwenye AMKA MTANZANIA kila siku, ambapo kwa sasa ni zaidi ya makala 1400, ELFU MOJA NA MIA NNE. Pia kwa email ambazo nimekuwa natuma kila wiki, kila wiki natuma email mbili mpaka tatu, kwa watu wasiopungua elfu nane. Kuiweka blog ya AMKA MTANZANIA hewani zipo gharama ambazo nalipia, kwa wewe kuweza kupokea email kila ninapotuma, zipo gharama ninazolipia kila mwezi. Hii ina maana unapokea email, sikuambii kwa namna yoyote ile ulipie, lakini mimi nailipia kuhakikisha unapata maarifa. Na unaweza hata usiijibu email yako, wala usiseme imekusaidia, au wakati mwingine ukaniambia nikutoe na nikakupa maelekezo ya kujitoa. Mambo yanakwenda hivyo.

Sasa unapotaka kuja kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambapo naweka kazi na gharama kubwa zaidi ya kutoa maarifa bora zaidi, ninakuomba uchangie gharama hizo, za kazi ninayofanya mimi kuhakikisha unapata maarifa, na pia gharama za kuendesha mitandao hii. Hii ina maana kwamba kwa kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, unawawezesha maelfu ya wengine kusoma AMKA MTANZANIA bure kabisa kila siku, na kupokea email bila ya kulipia chochote.

Hivyo basi rafiki, iwapo umekwama kweli na huwezi kushiriki semina inayokuja kwa kulipa ada ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, nakuelewa kabisa na nakusihi utembelee AMKA MTANZANIA, www.amkamtanzania.com kila siku uendelee kujifunza. Endelea pia kupokea email ambazo natuma kila wiki, ambazo zina kitu cha kukusaidia kupiga hatua.

Unapopata mafunzo hayo ya bure, yachukulie kwa umakini sana, yaone kama dhahabu, na kila unapofungua kusoma, andika kitu ambacho unatoka nacho na kwenda kukifanyia kazi. Ondoka na kitu ambacho utakitumia na utoke hapo ulipo sasa. Na kwa kufanya hivyo hutabaki hapo ulipo. Utaweza kulipia mafunzo mengine na kujifunza zaidi na zaidi.

Nikutakie kila la kheri rafiki yangu katika kujifunza, kama hutaweza kulipia semina basi endelea kujifunza, nitumie ujumbe wakati wowote kwenye email yangu ya makirita@kisimachamaarifa.co.tz ukiwa na changamoto yako na nitakusaidia bila ya gharama yoyote.

Kwa wale ambao wana uwezo wa kujiunga ila bado hawajafanya hivyo, nikukumbushe kwamba siku zimebaki chache sana, mwisho wa kujiunga ni tarehe 30/06/2017, zimebaki siku nne pekee. Ni vyema ukachukua hatua ya kujiunga leo.

Na mwisho kabisa, hata kama hujiungi kwa ajili ya semina, basi jiunge kama una uwezo huo, kwa sababu pia utakuwa umechangia gharama za kuendesha mitandao hii. Utakuwa umewawezesha wengine wengi kuendelea kupata maarifa haya bila ya kuyakosa.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ada ya mwaka tsh 50,000/= kwa namba zifuatazo; MPESA 0755 953 887, na tigo pesa 0717 396 253, airtel money tuma kwenda tigo pesa 0717 396 253. Ukishatuma ada, tuma ujumbe wenye majina yako kamili kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253. Karibu sana rafiki yangu, tuendelee kupata maarifa bora ambayo yatatuwezesha kupiga hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.